Kenya yatangaza ubinafsishaji wa makampuni yake ya serikali
Picha: Kenya yatangaza kubinafsisha baadhi ya makampuni yake ya serikali / Picha: ReutersNa Coletta Wanjohi
Kenya inatanguliza masoko ya mitaji kama mradi wa ukuaji
wa uchumi.
Uamuzi wa baraza la mawaziri mnamo tarehe 22 mwezi Machi,
uliidhinisha mswada mpya wa ubinafsishaji ambao utahusisha mali ya serikali
kuuzwa kwa sekta binafsi kupitia masoko ya mitaji ya nchi.
“Tutaorodhesha mali zinazomilikiwa na umma hivi
karibuni,” rais William Ruto alisema akiwa katika hafla kwenye soko la hisa la
Nairobi, siku ya Jumatano.
Baraza la mawaziri la Kenya limeidhinisha mswada mpya wa
Ubinafsishaji ambao utawezesha nchi kubinafsisha baadhi ya mashirika ya
serikali.
Mswada huo unapendekeza kwamba hazina ya kitaifa iunde na
kuendeleza mpango wa ubinafsishaji wa serikali na kuupitisha kwa baraza la
mawaziri ili kuidhinishwa. Mchakato huo hautaomba idhini ya bunge.
Mswada mpya ukiidhinishwa na bunge utachukua nafasi ya
sheria ya Ubinafsishaji ya mwaka 2005.
"Sheria iliyokuwepo hapo awali ilifanya iwe vigumu
kwa Wakenya kumiliki kipande chochote cha mali ya Kenya," rais alisema,
"kukiwa na sheria mpya tunaweza kuweka demokrasia kwa utajiri wetu na kuruhusu
mkenya kumiliki kipande cha kile ambacho ni cha nchi yake." William Ruto
Tume ya ubinafsishaji ya Kenya imetaja makampuni 25
zinazolengwa kwa ajili ya ugawaji wa fedha za serikali. Hizi ni pamoja na Benki
ya Maendeleo ya Kenya, Shirika la Agrochemical and Food Corporation, Mamlaka ya
Bandari ya Kenya, Kampuni ya Mafuta yani Kenya Pipeline Company na makampuni
kadhaa ya sukari.
Baadhi ya wataalam wa sheria, hata hivyo, wamekosoa
kipengele cha mswada huo uliolenga kuondoa bunge katika uamuzi kuhusu ubinafsishaji,
wakisema kuwa jukumu la bunge la usimamizi katika mchakato wowote ni muhimu.
