MPC YALAANI KITENDO CHA WAANDISHI WA HABARI KUCHEKELEA KUPEWA NYAMA NA MBUNGE
TAARIFA
KWA UMMA JUU YA UVUNJIFU WA MAADILI YA UANDISHI WA HABARI
Klabu
ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza (MPC), ni klabu iliyosajiliwa kwa
sheria ya Society Act Mwaka 1994 na kupewa namba ya usajili ya SO 8262, ikiwa
na dhima kuu ya kusimamia weledi wa uandishi wa habari ndani ya Mkoa wa Mwanza.
MPC
imefuatilia kwa ukaribu kusambaa kwa kipande cha picha nyongefu kikionesha
Mwandishi wa Habari Emmanuel Twimanye akimshukuru Hamisi Mwagao Tabasamu Mbunge
wa Jimbo la Sengerema kwa kutoa mgao wa nyama ya Mbuzi na Kondoo kwa baadhi ya
waandishi wa habari wa Wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, tukio lililotokea
Januari 1, 2024.
MPC
inalaani kitendo hicho kwa kuwa, kinakiuka misingi na maadili ya uandishi wa
habari kwani Mwandishi wa Habari hatakiwi kupokea pesa, zawadi au bakishishi
yoyote ile kutoka kwa Mwanasiasa, Afisa wa Serikali au Mfanyabiashara ili
kuepuka mgongano wa kimaslahi kwenye utendaji kazi wake.
MPC
inalaani kitendo hicho na imechukua hatua za kuwaonya waandishi wote
waliohusika kwenye tukio hilo na kuwaelimisha athari za vitendo hivyo kwenye
tasnia ya habari na mtazamo wa jamii na inawataka waandishi wote kuzingatia
maadili ya uandishi wa habari kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa
2024 na uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Ahsanteni
Edwin
C. Soko
Mwenyekiti,
MPC
02.01.2024

