Tanzania ina mpango wa
kusitisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili
kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao
ndani ya Ziwa hilo kubwa barani Afrika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katazo hilo litaanza Mei 15 Mwaka huu na kumalizika mwezi wa nane. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya
Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
"Pamoja na kufunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, Serikali imeanza
kutekeleza njia mbadala za kuwawezesha wananchi kujiendeleza kiuchumi katika Ziwa Tanganyika ikiwemo kukopesha vikundi, maboti na vizimba kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki na tayari imetenga shilingi milioni 200 kupitia Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi," alisema Waziri Ulega.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuweka katazo la muda la uvuvi kwenye moja ya maziwa yake. Mwanzoni mwa mwaka jana, Serikali ilisitisha uvuvi wa Samaki na viumbe wengine ndani ya Ziwa Viktoria kwa siku 15, ili kutoa fursa kwa dagaa kuzaliana zaidi, hasa kipindi cha mbalamwezi.
