BANDA MEDIA BLOG

Benjamin Mkapa yaanzisha matibabu ya moyo kutumia mishipa ya mikono

 

Matibabu ya moyo
Matibabu ya moyo

 ..............................................................

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma, nchini Tanzania, na mikoa iliyopo pembezoni mwa mji huo, wanaweza kunufaika na huduma mpya iliyoanzishwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya kufanya uchunguzi wa moyo kwa kutumia mshipa wa mkono.

Hii ni mara ya kwanza, kwa Hospitali hiyo kuanzisha huduma hii, ambayo wataalamu wanasema, njia hiyo inaweza kumpunguzia mgonjwa muda wa kukaa hospitali.

"Mgonjwa anarejea kwenye shughuli zake kwa wepesi na haraka ikilinganishwa na njia ya kupitia kwenye mshipa wa mguuni tuliyokuwa tukitumia wakiitumia awali," amesema Dk Kelvin Masava, ambae ni Mkuu wa Kitengo cha Maabara Maalumu ya Uchunguzi wa Moyo katika Hospitali hiyo.

Dk. Kelvin anasema kuwa utaratibu huo unamuwezesha mgonjwa kuweza kunyanyuka na kutembea mwenyewe mara tu baada ya kupata huduma tofauti na hapo awali ambapo mngojwa alilazimika kukaa siku kadhaa hospitali kwa ajili ya kujiuguza.

"Njia ya mshipa wa mguuni ilihitaji mgonjwa kukaa si chini ya saa sita baada ya huduma pasipo kuinuka kitandani au kukunja mguu tofauti na hii ambapo anainuka na kutembea mwenyewe na baada ya saa chache anaweza kuruhusiwa kwenda nyumbani siku hiyo hiyo," ameongeza.

Nchini Tanzania kumeshuhudiwa ongezeko la wagonjwa wa moyo kila mwaka. Katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani ya mwaka jana, Waziri wa Afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu, amekiri kuwepo kwa ongezeko la asimilia 9.4 ya wagonjwa wa moyo nchini humo.

“Takwimu za Wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS-2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa Moyo na Shinikizo la Damu kwa asilimia 9.4,” alisema Waziri Ummy.

Wakati huo huo, wananchi wametakiwa kutenga muda wa kufanya mazoezi kama njia moja wapo ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa moyo.

“Mtenge muda wa kufanya mazoezi japo dakika 150 kwa wiki na mazoezi haya siyo lazima yawe ya kukimbia yanaweza kuwa hata ya kutembea, kupima Afya japo mara moja kwa mwaka, kupunguza vilevi na kuacha kabisa matumizi ya tumbaku," ameshauri Waziri Ummy.

Wananchi pia wametakiwa kupunguza matumizi ya ziada ya chumvi, sukari na mafuta ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tatizo la moyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG