Waziri Mkuu wa Afrika Kusini ameonya uwezekano wa
kutokea majanga zaidi kama mazungumzo ya kumaliza mashambulizi dhidi ya Gaza
yatasimama.
Naledi Pandor aliliambia Shirika la Habari la Nchi
hiyo(SABC) siku ya Jumanne kuwa walikuwa wamemuomba balozi wao ndani ya Umoja
wa Mataifa kufanya jitihada za kuwashirikisha mabolizi wenzake kupitisha azimio
la kusitisha mapigano hayo.
“Kwa sasa, kila mtu aazimie kumaliza mashambulizi
hayo mara moja,” Pandor alisema.
Aliongeza kuwa dunia itashuhudia majanga zaidi kuliko
ya sasa, iwapo mashambulizi hayo hayatasitishwa.
'Hali tete'
“Ningetamani sana kuwatakia raia wa Palestina na
Waislamu wote Ramadhani yenye Baraka, lakini kwa watu wa Palestina, naona bado
hali ni tete iwapo dunia itaendelea kukaa kimya bila kuchukua maamuzi yoyote
kuhusu kumalizwa mara moja kwa mashambulizi haya,” alisema Pandor.
Mwanadiplomasia huyo amesema itakuwa ishara nzuri kwa
nchi zenye nguvu kama vile Marekani na Uingereza zitaungana na kuamua kupeleke
majeshi yao kuokoa maisha ya biandamu wa Gaza na raia wa Palestina kwa ujumla.
“Kwa wakati huu...bado nina wasiwasi kuwa tunaweza
kuendelea kushuhudia madhara zaidi kwa watu wa Palestina...ubinadamu wangu
unakosa maana iwapo tunashindwa kuwasaidia watu kutoka kwenye hali mbaya kama
ile,” alisema.
Afrika Kusini imelaani mashambulizi ya Israel katika
mji wa Gaza na kuishtaki nchi hiyo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ)
nchini Uholanzi.
Asilimia 85 wakosa makazi
Maamuzi ya muda mfupi ya Mahakama yaliyotolewa mwezi
Januari yameitaka Tel Aviv kuacha vitendo hivyo na kuchukua hatua madhubuti
zitakazotoa uhakika wa kutolewa kwa msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia wa
Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi dhidi ya ukanda wa
Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya kikundi cha Palestina cha Hamas kufanya
mashambulizi mpakani mwa Israel. Mashambulizi dhidi ya Gaza hadi sasa yameua
takribani watu 30,631 na kujeruhi wengine 72,043 huku kukiwa na uharibifu
mkubwa wa mali na upungufu wa mahitaji muhimu na huduma za kijamii.
Mapigano hayo yamewaacha zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa Gaza bila makazi, huku wakipitia uhaba wa chakula, maji safi na matibabu, wakati asilimia 60 ya miundombinu imeharibika, kulingana na Umoja wa Mataifa.
