Umoja wa Afrika (AU) umewatunuku nishani
ya heshima wanajeshi 21 kwa huduma yao chini ya Ujumbe wa Ufuatiliaji, Uhakiki
na Uzingatiaji wa AU (MVCM) ulio katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia
tangu Disemba 2022.
Jukumu lao lilianza baada ya serikali ya
Ethiopia na viongozi wa kikundi cha Tigray People's Liberation Front, TPLF
kutoka kaskazini mwa nchi waliotia saini makubaliano ya amani Novemba 2022.
Hii ilimaliza vita kati yao vilivyoanza
kati ya mwaka 2018 hadi 2020 ambapo watu takriban 600,000 walipoteza maisha, na
mamilioni wengine kulazimika kuhama makazi yao.
Wanajeshi 21 walitunukiwa nishani ya
heshima katika makao makuu ya Umoja wa Afrika Addis Ababa nchini Ethiopia.
Wanajeshi hao, ni kutoka Ethiopia, Kenya,
Nigeria, na Afrika Kusini na walisifiwa kwa kutekeleza majukumu yao kwa kwa
bidii, huku wakithibitisha na kuhakikisha uzingatiaji wa utekelezaji wa
Makubaliano ya Kudumu ya Kukomesha Uhasama (COHA).
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika
Moussa Faki Mahamat alisema wanajeshi wamesaidia "kufikia amani kupitia
mchakato ambao umesalia kuwa unaomilikiwa na kuongozwa na Ethiopia tangu
kusainiwa kwa Mkataba."
Majukumu yao yalijumuisha kufuatilia
mchakato wa upokonyaji silaha, kuwakomboa watu na kuwajumuisha tena katika
jamii (DDR), kuwapa makazi wakimbizi wa ndani, kurejesha huduma za kiuchumi na
kijamii, kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na ulinzi wa raia
katika eneo la Tigray.
"Tuzo munayopokea leo ni shukrani
kwa huduma kubwa mulizotoa na mutaendelea kutoa kwa Afrika yetu pendwa na watu
wake,” alisema Olusegun Obasanjo, rais wa zamani wa Nigeria, ambaye ni
Mwakilishi Mkuu wa AU katika Pembe ya Afrika na Mwenyekiti wa AU kuhusu
Mchakato wa Amani wa Ethiopia.
Ethiopia ni nchi ya kwanza kufaidika na
Mfuko wa Amani wa AU kwa kupokea dola za Kimarekani milioni 1 kwa ajili ya
kusaidia mchakato wake wa upokonyaji silaha, kuwakomboa watu na kuwajumuisha
tena katika jamii (DDR).

