Sasa ni rasmi.
Saulos Chilima, Makamu wa Rais wa Malawi amefariki
dunia kufuatia ajali ya ndege iliyotokea Juni 10, 2024.
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza kuwa
makamu wake Dkt Saulos Klaus Chilima na wengine tisa wamefariki dunia baada ya
ndege waliyokuwa wanasafiria kuanguka katika msitu wa Chikangawa katika eneo la
Mzimba, nchini Malawi, Juni 10, 2024.
Chilima, na wengine tisa walikuwa wameabiri ndege ya
Jeshi la Ulinzi la Malawi (MDF) iliyoripotiwa kutoweka kwenye mawasiliano ya
rada mara baada ya kushindwa kutua kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mzuzu siku
ya Jumatatu.
Ndege hiyo iliruku kutoka uwanja wa ndege wa Mzuzu
saa moja na dakika tano asubuhi ya Jumatatu na kutua katika uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kamuzu mjini Lilongwe, kisha ikamchukua Makamu wa Rais, tayari
kurudi Mzuzu.
Ndege hiyo pia ilikuwa imembeba Shanil Muluzi, mke wa
rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi . Walikuwa wanaenda katika ibada ya
mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Sheria Ralph
Kasambara aliyefariki siku ya Ijumaa.
Chilima ni nani?
Mtaalamu huyo wa uchumi alizaliwa Februari 12, 1973
Chilima alipata shahada ya Uzamivu katika Usimamizi wa Maarifa kutoka Chuo
Kikuu cha Bolton nchini Uingereza.
Kabla ya kuingia katika siasa, Chilima alianzia
kwenye sekta binafsi na kushika nafasi za juu katika kampuni mbali mbali
yakiwemo Airtel Malawi na Unilever.
Aliingia rasmi kwenye siasa akiwa mgombea mwenza wa
Peter Mutharika katika uchaguzi wa urais wa 2014, ambapo walishinda na
akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Chilima alijizolea sifa kutokana na mageuzi yake ya kiuchumi katika nchi hiyo, ikiwemo kupambana na ufisadi.
Mwaka 2018, alianzisha Umoja wa Mageuzi (UTM) baada
ya kutofautiana na Rais Mutharika na Chama cha Maendeleo cha Kidemokrasia
(DPP).
Aligombea urais katika uchaguzi wa 2019 lakini
hakushinda.
Hata hivyo, katika marudio ya uchaguzi wa urais wa
2020, alichaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais baada ya kupita kama mgombea mwenza
wa Rais wa sasa, Lazarus Chakwera.
Ajali za anga hivi karibuni
Hii si mara ya kwanza kwa ndege na helikopta za
viongozi kupotea na kisha kuripotiwa kupata ajali.
Mwezi uliopita, helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa
Iran Ebrahim Raisi ilianguka kufuatia hali mbaya ya hewa. Kiongozi huyo
alipoteza maisha akiwa na ujumbe wake.

