Kikosi cha Somali kimekuwa kikipigana na wanamgambo wa Alshabab kwa zaidi ya miaka 16. /Picha: Wengine
Serikali ya Somalia ilisema wanajeshi wake watano
walikufa katika vita, huku wakiwaua karibia wapiganaji 50 kutoka kundi la
wanamgambo la Al-Shabaab siku ya Jumamosi, takriban kilomita 350 kaskazini mwa
mji mkuu, Mogadishu.
Wanajeshi wa serikali na vikosi vinavywaunga mkono
walipata taarifa za shambulio lililopangwa na Al-Shabaab huko Ceeldheer, katika
eneo la Galgadud, na hivyo kuwavizia, na "kuwaangamiza", ilisema
taarifa.
Kulingana na mamlaka, vikosi vyao viliwauwa takriban
wanachama 47 wa kundi la wanamgambo huku wakiwapoteza wanajeshi watano katika
vita hivyo. Walisema mashambulizi ya anga pia yalitekelezwa dhidi ya vikosi vya
Al-Shabaab.
Al-Shabaab walidai kuhusika na shambulio la
Ceeldheer.
'Mapigano makali'
Mkazi wa eneo hilo Mohamed Hussein aliiambia AFP kwa
simu: "Kulikuwa na mapigano makali katika mji wa Ceeldheer asubuhi ya leo
baada ya Al-Shabaab kushambulia mji huo kutoka pande kadhaa.
"Ilikuwa vigumu sana kusema ni nani alikuwa
akitawala muda mfupi uliopita, lakini sasa tunaweza kuona kwamba vikosi vya
serikali ya Somalia viko katika udhibiti kamili," aliongeza.
Mwanmaume mwingine wa eneo hilo, Hassan Gutale,
alisema, "Kulikuwa na milipuko mikubwa isiyopungua sita na mapigano ambayo
yalichukua saa kadhaa."
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa
Mei 2022, aliapa kuanzisha "vita kamili" dhidi ya kundi hilo la
wanamgambo.
Vita dhidi ya Alshabab vinaendelea kwa
muda mrefu
Al-Shabaab imekuwa ikiendesha uasi mbaya dhidi ya
serikali kuu dhaifu huko Mogadishu kwa zaidi ya miaka 16.
Ingawa walifukuzwa nje ya mji mkuu na kikosi cha
Umoja wa Afrika mwaka 2011, bado wana uwepo mkubwa katika maeneo ya vijijini
nchini Somalia.
Wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara
dhidi ya wanasiasa, walinzi wa usalama na raia, hasa nchini Somalia lakini pia
katika nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Kenya.
Serikali hio inayokabiliwa na hali ngumu nchini
Somalia imeungana na wapiganaji wa makabila dhidi ya waasi hao, na kufaulu
kudhibiti tena maeneo mengi katikati mwa Somalia, katika operesheni inayoungwa
mkono na ujumbe wa AU unaojulikana kama ATMIS pamoja na mashambulizi ya anga ya
Marekani.
Lakini mashambulizi hayo yamekabiliwa na vikwazo,
huku Al-Shabaab mapema mwaka huu wakidai kuwa imedhibiti maeneo mengi katikati
mwa nchi.
