Wanandugu wa waathirika wa ajali hiyo walikuwepo kwenye uwanja wa ndege wa mjini Lilongwe kupokea miili ya wapendwa wao. Picha/Serikali ya Malawi
Malawi imetangaza siku 21 za maombolezo kufuatia kifo
cha Makamu wa Rais wa nchi hiyo Saulos Chilima na watu wengine nane kilichosababishwa na ajali
ya ndege.
Mabaki ya ndege hiyo yalipatikana siku ya Jumanne,
ndani ya msitu mnene na wenye vilima vikali karibu na mji wa Mzuzu.
Kipindi cha maombolezo kinaanza Juni 11 mpaka Julai
1, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limesema katika taarifa yake ya Jumanne.
Bendera kupepea nusu mlingoti
Rais Lazarus Chakwera ameelekeza bendera zote kupepea
nusu mlingoti wakati wote wa maombolezo, iliongeza taarifa hiyo.
Kulingana na baraza hilo, taratibu za mazishi
zitatangazwa hapo baadaye.
Mabaki ya miili ya Chilima na waathirika wengine
ilisafirishwa kwa ndege kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.
Rais Chakwera aliambatana na viongozi wengine wa
serikali kuipokea miili hiyo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kamuzu,
jumanne jioni.
Baadhi ya viongozi mbalimbali ulimwenguni wameendelea
kutuma salamu zao za rambirambi kwa familia na serikali ya Malawi.
