Na Rose Jacob,MWANZA.
MWANAMUME mmoja aliyefamika kwa majina ya Samwel Anthony,(34) mkazi wa kijiji cha Shilima,amehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Kwimba kifungo cha maisha jela kwa kubaka mtoto wa miaka 8.
Hukumu hiyo imetolewa leo Novemba 20 mwaka huu, hakimu mkazi Mkuu Ndeko Dastan,ambaye ndio hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, baada ya kusikiliza mashahidi 5 wa Jamhuri akiwemo mhanga,hivyo mahakama imejiridhisha kuwa mtuhumiwa ametenda kosa hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo,ilieleza mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo Agasti 16.08 mwaka huu, huko maeneo ya kijiji cha Shilima, wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Mhanga ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kisheria, alifanyiwa kitendo hicho wakati ameagizwa na mama yake dukani,wakati anarudi ndipo mtumiwa alimvuta nyuma ya nyumba ya baba wa mhanga kisha kumfanyia ukatili huo.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani Agasiti 23 mwaka huu,kusomewa shtaka la kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) na 131 (3) vya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 ya Sheria marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa ameiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye mwenyewe ni mgonjwa wa mapafu, ana watoto watano mmoja mlemavu na pia anamlea mdogo wake ambaye naye ni mgonjwa pia mkewe amemuachia mzigo mkubwa wa kulea hiyo familia ni kubwa.
Licha ya Mshtakiwa kuiomba mahakama impunguzie adhabu, hakimu Ndeko amesema kwamba mahakama hiyo imefungwa mikono kwani kifungu cha 131 (3) cha Kanuni ya Adhabu ambacho mtuhumiwa ameshtakiwanacho kinatoa adhabu ya kifungo cha maisha na hakijampa hakimu kubadili adhabu hiyo.
Mwisho.
.jpg)