Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt, Damas Ndumbaro wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza. Wengine ni Watendaji wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa hicho kilichopo Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza
Na Veronica Mwafisi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora-Mwanza
Tarehe 15 Machi, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeelekeza nyaraka kuhifadhiwa katika mfumo wa kidijiti ili kuwezesha kizazi cha sasa kujua historia ya nchi na kulinda amani kwa maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 15 Machi, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.
Akitoa maelekezo hayo kwa niaba ya kamati yake, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kizazi cha sasa kutokujua historia ya nchi yao kumesababisha kutoona umuhimu wa kuitunza amani ya nchi.
“Kuna umuhimu sasa yale mambo ya kihistoria ambayo siyo nyeti tuyachambue ili yawafikie vijana, tujivunie utaifa wetu, tusisubiri watoto wetu wafunzwe na ulimwengu, tuwawekee nyaraka zitakazosaidia kujua historia ya nchi yao kwenye mfumo wa kidijiti. Mhe. Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Aidha, kamati hiyo imempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Bw. Firimin Msiangi pamoja na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Kazi nzuri sana imefanyika, tumeona, changamoto ya bajeti mliyonayo tunamuelekeza Waziri ifanyiwe kazi kwa kutoa kipaumbele kwenye kuziweka nyaraka katika mfumo wa kidijiti na masilahi ya watumishi wa Idara hii nyeti, ameongeza Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa wajumbe wa kamati hiyo kuitumia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kujifunza historia ya nchi na kuona nyaraka ambazo zitawasaidia katika shughuli zao hasa kwa wanaohitaji kuandika vitabu.
“Kituo hiki kina utajiri wa kumbukumbu na nyaraka, kwa wanaotaka kujifunza historia ya nchi yetu na kuandika vitabu, mtumie kituo hiki, tumeona nchi hii ilivyo na historia ndefu, mtapata taarifa nyingi. Mhe. Kikwete amesisitiza.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakimsikiliza Afisa Kumbukumbu, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka, Bi. Maryam Ayoub (wa kwanza kushoto) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu Vita vya Kagera kwa Wajumbe hao wakati wa ziara ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza
Vile vile Mhe. Kikwete amewasisitiza wajumbe hao wa kamati kujifunza kuweka kumbukumbu zao na kuwarithisha vizazi vijavyo. Wenzetu huko nyuma walikuwa wanaandika na ndio maana tumeweza kuona historia nzuri ya nchi yetu, basi sasa nasi tujifunze kufanya hivyo kwa vizazi vyetu vijavyo, Mhe. Kikwete ameongeza.
Akiwasilisha taarifa ya Mradi wa Kituo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi alisema lengo la uanzishwaji wa kituo hicho ni kusogeza huduma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taasisi za serikali kwa Kanda ya Ziwa ili kulinda urithi wa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (wa kwanza kushoto) akifuatilia jambo pamoja na Wajumbe wa Kamati yake walipokuwa wakipatiwa maelezo mbalimbali ndani ya ghala la kuhifadhia nyaraka wakati wa ziara ya kikazi katika Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mradi wa kituo hicho kilichopo Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza.
