Mtaalamu mashuhuri wa magonjwa ya akili nchini Urusi ameainisha ushoga na utambulisho wa jinsia tofauti (transgender) kama magonjwa ya akili wakati wa kongamano kubwa la kitabibu nchini humo.
Akizungumza katika Kongamano la 18 la Wataalamu wa Magonjwa ya Akili wa Urusi wiki iliyopita, Olga Bukhanovskaya, daktari mkuu wa Kituo cha Kisayansi cha Matibabu na Ukarabati cha Phoenix mjini Rostov-on-Don, alianzisha dhana ya “ugonjwa wa wigo wa transgender.”
“Ikiwa watu sasa wanatumia kauli nzuri ya ‘ugonjwa wa wigo wa tawahudi (autism spectrum disorder),’ basi tunaweza kusema ‘ugonjwa wa wigo wa transgender,’ na magonjwa haya yote ya akili yanaingia humo,” alisema Bukhanovskaya.
Kundi hilo lililopendekezwa linajumuisha hali tano tofauti: “ushoga,” “fetishistic transvestism,” ambayo ni kuvaa mavazi ya jinsia tofauti kwa ajili ya msisimko wa kingono, “matatizo ya utu,” “ugonjwa wa schizotypal,” na “schizophrenia yenye tabia za kike za vipindi,” inayomaanisha tabia au mienendo ya kike inayojitokeza mara kwa mara kwa wanaume.
Aliwashutumu kile alichokiita “safu ya tano ndani ya tiba” kwa kuendeleza haki za watu wa transgender, akisema kuwa “madaktari, wanasaikolojia na wahadhiri wanaounga mkono trans-LGBT” wanawafundisha wagonjwa pamoja na jamii pana ya kitabibu mitazamo hiyo.
Shirika la afya dunianin liliondoa ushoga kwenye orodha yake ya matatizo ya akili mwaka 1990. Chini ya Mfumo wa Kimataifa wa Uainishaji wa Magonjwa (ICD-11) wa WHO, ambao hutumiwa na madaktari na mifumo ya afya duniani kote, hali ya transsexualism pia iliondolewa kwenye kundi la magonjwa ya akili wakati viwango vipya vilipoanza kutumika mwaka 2022.
Moscow ilisimamisha mpango wake wa kuhamia ICD-11 mwaka 2024, ikisema baadhi ya vipengele vyake vinakinzana na maadili ya jadi ya nchi hiyo.
Mwaka 2023, baada ya Urusi kupitisha sheria inayopiga marufuku “matibabu yanayolenga kubadili jinsia,” Jumuiya ya Wataalamu wa Magonjwa ya Akili ya Urusi iliandaa mwongozo wa kitabibu kuhusu “matatizo ya utambulisho wa kijinsia.” Waraka huo ulitambua kuwa watu wa transgender hawawezi “kutibiwa” na badala yake ukapendekeza msaada wa tiba ya kisaikolojia.
