
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Machano Ali Machano (katikati)
Na Mwadishi wetu, Arusha
Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Machano Ali Machano, amesema bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya mwaka huu imejengwa katika msingi wa kutekeleza malengo ya waanzilishi wa jumuiya hiyo huku ikilenga moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi wa nchi wanachama.
Machano, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya EALA, amesema mchakato wa maandalizi ya bajeti umeenda vizuri tangu ngazi ya wataalamu hadi hatua ya kujadiliwa bungeni, ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo tayari amewasilisha ripoti yake na wabunge wanaendelea kuijadili.
Amesema hatua hiyo inaonesha namna taasisi za jumuiya zilivyojipanga kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaendana na malengo ya msingi ya EAC.
Amefafanua kuwa kamati ya bajeti ilijikita kuangalia historia, madhumuni na makusudio ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuhakikisha bajeti inayopitishwa inaleta matokeo yanayotarajiwa.
Kwa mujibu wake, bajeti hiyo imekuwa ya mafanikio kwa kuwa imezingatia vipaumbele vya taasisi mbalimbali za jumuiya, zikiwemo zile zinazohusika na maendeleo ya lugha ya Kiswahili, uchumi, na ustawi wa wananchi wa ukanda huo.
Machano amesema katika kipindi hiki cha mabadiliko ya dunia na maendeleo ya teknolojia, bajeti za jumuiya haziwezi kubaki katika muundo wa zamani, bali zinapaswa kuendana na hali halisi ya sasa.
Amesema bajeti ya mwaka huu imezingatia changamoto na mahitaji ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa kuangalia zaidi maisha ya kila siku ya watu wa kawaida, hususan vijana na wanawake ambao wanahitaji fursa za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amempongeza Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rebecca Kadaga, kwa kusimamia vizuri ajenda za jumuiya na kuweka msukumo katika utekelezaji wa mipango iliyopitishwa.
Amesema taasisi zote za EAC zimeanzishwa kwa kuzingatia mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, hivyo ni wajibu wa kila chombo kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kupitia bajeti zinazolenga maendeleo ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Tags
BUNGE EAC