
Ushirikiano wa muda mrefu wa miaka 65 kati ya Tanzania na Italia umeendelea kuwa mfano wa mahusiano ya kidiplomasia yaliyojengwa katika misingi ya urafiki, kuheshimiana na ushirikiano wa kimkakati katika nyanja za maendeleo, diplomasia na utamaduni. Hali hiyo ilidhihirika tena katika sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Italia iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Italia, barabara ya Tanzanite jijini Dar es Salaam, Juni 02, 2026.
Katika hafla hiyo iliyopambwa kwa hadhi ya kipekee, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Uvuvi, Dkt. Bashiru Kakurwa, ambapo pamoja na wageni mbalimbali walioshiriki wakiwemo wawakilishi wa Serikali ya Tanzania, mabalozi wa nchi mbalimbali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, walijumuika kuadhimisha historia ya taifa hilo pamoja na kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Italia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, H.E. Giuseppe Seán Coppola, alisema kuwa mwaka huu una uzito wa kipekee kutokana na kuadhimishwa kwa miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Italia mwaka 1946, sambamba na miaka 65 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Italia na Tanzania.
Alibainisha kuwa katika kipindi chote hicho, nchi hizo mbili zimeendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, uchumi, utamaduni na diplomasia ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa mahusiano hayo yamejengwa juu ya msingi imara wa kuheshimiana na kuaminiana.
Balozi Coppola alieleza pia kuwa diplomasia ya utamaduni bado ni nguzo muhimu inayochochea uelewano na kuimarisha urafiki kati ya mataifa hayo mawili, akibainisha kuwa matukio ya kitamaduni yana nafasi kubwa ya kuwaleta watu karibu zaidi kuliko mipaka ya kijiografia.
Hafla hiyo ilipambwa na burudani ya kipekee kutoka kwa kundi la muziki wa jadi la Italia “Officina Zoé”, ambalo lilionesha umahiri wa muziki na dansi za jadi za “Pizzica” kutoka Italia ya Kusini, na kuvutia wageni wote waliohudhuria.
Kama sehemu ya maadhimisho mapana, Ubalozi wa Italia kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chuo cha Muziki cha Dhow Countries Music Academy, umetangaza kuandaa maonesho mawili maalum ya kikundi hicho huko Zanzibar, yatakayolenga kuendeleza zaidi ushirikiano wa kitamaduni kati ya Tanzania na Italia.
Maadhimisho hayo yameendelea kuonesha umuhimu wa uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Italia, ukiwa ni mfano wa diplomasia inayolenga kuimarisha mshikamano wa kimataifa, amani na maendeleo endelevu kupitia ushirikiano wa kweli wa mataifa.
