BANDA MEDIA BLOG

CCT YAZINDUA JENGO LA ZAIDI BILLIONI 3. JIJINI DODOMA

 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kukuza sekta binafsi, ikiwemo uwekezaji unaofanywa na Taasisi za Dini kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi.

Senyamule ameyasema hayo  Julai 09, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la kitega uchumi la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT Complex), hafla iliyoambatana na Mkutano wa 60 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo, uliofanyika katika ukumbi uliopo ndani ya jengo hilo.





"Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kukuza sekta binafsi, ikiwemo Taasisi za Dini. Tunatambua mchango mkubwa wa taasisi hizi katika utoaji wa elimu, huduma za afya, kujenga maadili ya jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi," amesema 

Ameongeza kuwa miradi ya uwekezaji kama huo ni mfano mzuri wa namna Taasisi za Dini zinavyoweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa kupitia uanzishaji wa vitega uchumi vinavyozalisha ajira, kuongeza mapato na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi. Aidha, amesema uwekezaji huo unaakisi maono yenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dkt. Stanley Hotay, amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika safari ya Jumuiya hiyo kuelekea kujitegemea na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje. Amesema kupitia uwekezaji huo, CCT imeongeza uwezo wake wa kuzalisha mapato ya ndani, ambapo hadi kufikia Juni 2026 kiwango cha kujitegemea kimeongezeka hadi asilimia 33 kutoka asilimia 20 iliyokuwepo wakati wa tathmini ya awali mwaka 2025.


Naye Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Dkt. Moses Matonya, amesema jengo hilo la uwekezaji linaisaidia Jumuiya kujijengea uwezo wa kifedha, huku likichangia pia kuwahudumia wananchi kupitia kuimarisha shughuli za uinjilishaji katika maeneo mbalimbali ya Nchi pamoja na utoaji wa huduma za kijamii zinazotekelezwa na Jumuiya hiyo.

Mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la CCT ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026. Umegharimu shilingi bilioni 3.8 na hadi sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji. Jengo hilo linatarajiwa kuingiza mapato ya takribani shilingi milioni 600 kwa mwaka, huku likiwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 500 katika kumbi zake. 














Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG