BANDA MEDIA BLOG

DCEA YAKAMATA TANI 22.6 ZA DAWA ZA KULEVYA NDANI YA MIEZI MIWILI

 

Emmanuel Alphonce Kiligi Meneja wa ukaguzi na udhibiti wa Dawa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA). 

Nuru Edgar Mwasulama Meneja Ukaguzi na Utekelezaji Sheria Shirika la Viwango Tanzania TBS. 

…………… 

Na John Bukuku, Dar es Salaam

Julai 2, 2026 – Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata tani 22.6 za dawa za kulevya katika operesheni mbalimbali zilizofanyika nchini kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu, huku watuhumiwa 188 wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni za ndani na ushirikiano wa kimataifa uliowezesha kuvunja mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya.

Alisema katika kipindi hicho DCEA ilikamata tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 11.63 za heroini, kilogramu 40 za skanka pamoja na lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya.

Aidha, mamlaka hiyo iliteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi katika wilaya za Chamwino mkoani Dodoma, Kilwa mkoani Lindi pamoja na Sengerema mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti uzalishaji wa dawa hizo nchini.

Lyimo alisema miongoni mwa mafanikio makubwa ya operesheni hizo ni kukamatwa kwa tani 2.6 za mirungi katika eneo la Tarakea mkoani Kilimanjaro, zikiwa zimetokea Kenya na kusafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso kabla ya kukamatwa Mbezi Makonde, Dar es Salaam.

Alisema watuhumiwa kadhaa walikamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku mtu mmoja akitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na mtandao huo wa usafirishaji wa dawa za kulevya.

Katika operesheni nyingine zilizofanyika jijini Dar es Salaam, DCEA ilikamata kilogramu 19.94 za bidhaa zilizokuwa zimefichwa katika vifungashio vilivyoonekana kuwa virutubisho vya lishe aina ya AFACELL (Moringa Extract), lakini baada ya uchunguzi wa maabara kubainika kuwa zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya dawa za kulevya aina ya Prazepam.

Kamishna Lyimo alisema bidhaa hizo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zinaandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Alionya kuwa matumizi holela ya dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya kama Prazepam bila ushauri wa daktari yanaweza kusababisha uraibu, kuharibika kwa mfumo wa fahamu, matatizo ya upumuaji, kupoteza fahamu na hata kifo.

Aidha, alisema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), DCEA ilibaini uwepo wa baadhi ya vinywaji aina ya energy drinks vilivyokuwa na kemikali ya THC, ambayo ni kiambata kinachopatikana kwenye bangi na kina madhara mbalimbali ikiwemo kuathiri afya ya akili, mfumo wa fahamu na kuongeza vitendo vya uhalifu.

Lyimo alisema DCEA pia imeimarisha ushirikiano wa kiutendaji na mamlaka za nchi za Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia na Kenya katika kukabiliana na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya, huku operesheni za pamoja zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na biashara hiyo.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya ili kulinda afya, usalama na ustawi wa jamii.       

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG