Na Maiko Luoga – DMK – Arusha
Wakristo wametakiwa kudumu katika maombi nyakati zote ili kuimarisha Imani na uhai wa Kanisa la Mungu na kuacha mazoea ya kuomba wakati wa changamoto pekee.
Wito huo umetolewa Jumamosi Tarehe 27 Juni 2026 na Askofu Stanley Hotay, wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK) Kanisa Anglikana Tanzania na Mwenyekiti Jumuiya ya Kikristo Tanzania CCT.
Askofu Hotay alitoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Mtandao wa wanamaombi wa Kanisa Anglikana (Anglican Prayer’s Network – APN) uliofanyika katika Chuo cha Biblia Mungu Ishi Arusha, na kuhudhuriwa na Timu ya waombaji kutoka Kanisa Anglikana Tanzania na Kenya.
“Kanisa linahitaji watu wanao simama katika maombi, hatua ya kwanza unapoamka Asubuhi ni lazima kuanza na maombi kuombea Kanisa, Familia, Jamii na Taifa ili kujenga msingi imara” alisema Askofu Hotay.
Washiriki wa Kongamano hilo kutoka Kenya na Tanzania wameungana kuomba kwaajili ya Kanisa na amani ya Mataifa yao, nchi za Afrika pamoja na kufanya maombi maalumu kwaajili ya Chuo cha Biblia Mungu Ishi ili kiendelee kuwa eneo muhimu la kuzalisha watumishi wa Injili ya Kristo.
Katika Kongamano hilo imetangazwa kazi ya kutafuta Gari ya huduma ya Idara ya Utume na Uinjilisti ya Kanisa Anglikana Tanzania na Kasisi Obedi Chikoga kutoka Dayosisi ya Morogoro ametangazwa kuwa Mwenyekiti.
Mratibu wa Idara ya Utume na Uinjilisti, Kanisa Anglikana Tanzania Kasisi Can. Linus Burian amesema, kupitia washiriki wa Kongamano hilo tayari ahadi ya Fedha kiasi Tsh. 32,600,000/= (Milioni thelathini na mbili na laki sita) zimepatikana.
Kongamano hilo limepangwa kufanyika tena Tarehe 24 hadi 28 Novemba 2026 katika Kanisa Anglikana ACK Dayosisi ya Malindi nchini Kenya, Askofu Moses Masamba Dean ACK ametumia nafasi hiyo kuwaalika watu wote kutoka Tanzania kujiandaa ili kufika nchini Kenya kushiriki Kongamano hilo.


