Na. Rahma Magona, DODOMA
Stendi ya Mabasi ya Jiji la Dodoma iliyopo Nzuguni inatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa katika kuongeza ufanisi wa uendeshaji, uboreshwaji wa huduma na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Hatua hiyo imekuja leo baada ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya ukaguzi katika kituo cha mabasi kwa lengo la kubaini changamoto zinazochangia kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Bakari Fundikila, alisema kuwa kupitia vikao vya fedha na uongozi, Halmashauri imeazimia kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika kituo hicho, hivyo wamepanga kukutana na wadau wa mabasi ili kupata ushauri kuhusu namna bora ya kupanga maeneo ya kuweka mabasi yaani terminal.
Fundikira alisisitiza kuwa moja ya mikakati ya Jiji ni kuhakikisha mabasi yote yanaelekezwa kutumia kituo cha Mabasi ya Jiji la Dodoma badala ya stendi zilizopo mitaani, hatua inayolenga kuboresha usimamizi wa usafirishaji na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Nae,Kaimu Mkrugenzi Charity Sichona alisema kuwa maoni yaliyotolewa yatachukuliwa na kufanyiwa kazi, huku akiahidi kufanya mabadiliko makubwa katika stendi hiyo kupitia mifumo mipya ya uendeshaji na kuboresha miundombinu.
Aidha, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Halmashauri ya kutathmini miradi yenye uwekezaji mkubwa lakini mapato yake hayajaendana na uwekezaji huo, kwa lengo la kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuongeza tija na mapato.

