Rais mteule wa Tanzania John Pombe
Magufuli ameapishwa leo baada ya ushindi wake katika uchaguzi uliotajwa
kuwa wenye ushindani zaidi katika historia ya Tanzania.
Akijulikana
kama ‘Tingatinga’, Magufuli alishinda kwa kupata asilimia 58.46 ya kura
huku hasimu wake mkubwa Edward Lowassa akipata asilimia 39.97 ya kura.Ushindi wa Magufuli ulipokelewa kwa hisia tofauti, kwani hata kama kura nyingi za maoni zilionyesha kuwa angeshinda, wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa walikuwa na wakati mgumu kubashiri nani hasa atashinda hasa wakizingatia namna ushindani ulivyokuwa mkali baada ya vyama vinne vya upinzani kuungana na kumsimamisha Lowassa kama mgombea wao wa Urais.
Kwa kiasi kikubwa, Magufuli alibebwa na umaarufu wake binafsi zaidi ya ule wa chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwepo madarakani tangu uhuru wa Tanzania mnamo mwaka 1961, ingawa kilipata jina la sasa 1977 baada ya kuungana kwa Tanu na chama cha Afro Shirazi cha Zanzibar.
Uchaguzi umekwisha sasa, kazi imebaki kwa mtu mmoja, Magufuli. Ama kwa hakika yapo mambo lukuki yanayohitaji uongozi wake uyashughulikie, lakini yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo ushughulikiaji wake ndio utakaopelekea namna uongozi wake utakumbukwa hapo baadaye, kama anavyochanganua mwandishi wa BBC Sammy Awami.
1. Rushwa
Mabadiliko’ ni neno lililotawala kila kona wakati wa pilika pilika za kampeni, katika kambi za upinzani na hata chama tawala.
Na sasa kwa kuwa Magufuli ndio amepewa jukumu kuongoza nchi, Watanzania wanategemea kazi ya kwanza atakayoifanya ni ‘kusafisha nyumba’.
Akiwa kama ‘mkuu wa kaya’, Magufuli anatarajiwa kuweka kipaumbele katika kuwashughulikia wala rushwa na mianya ya rusha yenyewe.
Bila shaka hii haitakuwa kazi rahisi. Wapo viongozi wengi wa umma na wale wa chama chake ambao kuwa kwao madarakani kwa muda mrefu kumewawezesha kujijengea mazingira ya kujinufaisha bila kuwa na wasiwasi wa kugundulika na kuadhibiwa.
Lakini tangu siku ya uzinduzi wa kampeni, Magufuli mwenyewe aliahidi kwamba ataanzisha mahakama maalum ya rushwa ili mafisadi wadhibitiwe ipasavyo na kwa kasi itakayoridhisha. Na kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa kwake kumetokana na imani ya Watanzania wengi kwamba anayo nia ya kupambana na hali ya rushwa iliyokithiri
Kipimo cha kwanza kabisa kitakuwa katika uundwaji wa baraza lake la mawaziri. Je, litahusisha watu ambao hawana madoa ya rushwa? Watakuwa ni watu wenye sifa ya uchapakazi? Bila shaka haya ndio maswali yanayogonga vichwa vya wananchi wengi hivi sasa.
Kwa hakika utakuwa ni mtihani wake mgumu wa kisiasa, lakini wengi wa waliompigia kura wanaamini kwamba anauthubutu wa kufanya maamuzi magumu
2. Vijana na Ajira
Vijana wamefanyika chachu kubwa sana katika uchaguzi huu ulioisha. Wengi wao waliamini kwamba kura yao ni ya muhimu na ina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko. Na si vigumu sana kujua kwa nini vijana hawa walihamasika kiasi hicho.
Takribani nusu ya Watanzania zaidi ya milioni 50 ni vijana, na hili ndio kundi linaloathirika zaidi na ukosefu wa ajira nchini
Takwimu rasmi za serikali zinasema ukosefu wa ajira upo kwa asilimia 10, lakini mara nyingi watu hudhani tatizo ni kubwa zaidi ya hapo.
Wengine watakumbuka lile tangazo la kazi la siku chache zilizopita katika idara ya uhamiaji. Kwa nafasi 70 za kazi, maombi yaliyopatikana yalikuwa 10,000. Hata udahili ilibidi ufanyike katika uwanja wa taifa wa mpira.
Magufuli anabeba mzigo mkubwa wa kuhakikisha vijana hawa wengi waliojitokeza kupiga kura wanafunguliwa milango ya kupata nafasi za ajira. Labda kupitia ahadi yake ya kufufua na kuanzisha viwanda vipya inaweza kutatua uhitaji huu
3. Elimu
Wakati upinzani ukiahidi elimu ya bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, Magufuli yeye aliahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari, kidato cha nne tu.
Elimu ni moja ya ahadi ambazo ziliwekewa mkazo na pande zote mbili za ushindani hali inayoonesha uhitaji mkubwa uliopo katika sekta hii.
Wakati Watanzania wengi wakifurahishwa na ahadi ya elimu bure, wengi wao pia hawaridhishwi na ahadi hiyo kuishia hapo tu.
Walimu na maslahi yao, kiwango cha elimu kisichoridhisha, mitaala isiyozalisha wahitimu wenye ujuzi wa kutosha kwa nguvu kazi ya taifa lakini hata ushindani wa nje ya nchi.
Shule nyingi za umma hazina walimu wa kutosha na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Magufuli anakabiliwa na changamoto ya kuyatatua haya na mengine kadhaa kuhusiana na sekta ya elimu.
4. Katiba Mpya
Tags
HABARI KITAIFA





