| Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said akizungumza katika mkutano huo. |
| Kamanda wa Ulinzi na Mazingira wa Soko hilo, Nurdin Hassan akisisitiza jambo kuhusu wanavyo imarisha ulinzi katika soko hilo. |
| Mama Lishe wa soko hilo, Taus Barnabas, akichangia neno katika mkutano huo. |
| Mama Lishe wa soko hilo, Fatuma Saijali (katikati), akizungumza katika mkutano huo. |
Mwonekano wa sehemu ya soko la Samaki la Feri
Na Dotto Mwaibale
ENEO la Lebanon katika Soko la Kimataifa
la Samaki la Feri ambalo lipo jirani na Ikulu jijini Dar es Salaam
limedaiwa kuwa ni hatari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kuwa
linadhohofisha uchumi kutokana na kukithiri kwa watu wasio rasmi.
Hayo yamebainishwa na Mwezeshaji wa
Sheria wa soko hilo, Asha Malenda wakati akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam leo asubuhi wanaotembelea masoko mbalimbali ya
Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia
umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG)
kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko hayo.
"Tunachangamoto kubwa sana katika soko
letu la Feri tunayoipata kutoka eneo la Lebanon lenye mwingiliano wa
watu wasio rasmi kutoka nje ya soko ambao ni kama wamejianzishia soko
lao na wamekuwa na maamuzi yao lakini viongozi wa soko la Feri
wanashindwa kuwachukulia hatua hali ambayo inatudhalilisha sisi
wafanyabiashara hasa mama lishe na kuharibu uchumi wa soko letu" alisema
Malenda.
Alisema wengi wa watu waliopo katika
eneo hilo lisilo rasmi wamekuwa wakifanya biashara kiholela huku
wakipika vyakula katika maeneo yanayoweza kuhatarisha afya ya mlaji
wakati katika soko hilo kuna eneo maalumu la mama lishe na wengi wa watu
hao wakienda kula eneo hilo rasmi wamekuwa hawalipi fedha na wakibanwa
kulipa wanadiliki kutoa visu na silaha za jadi kuwatishia wanaodai.
"Eneo hilo la Lebanon ni hatari na
kinachoshangaza linatizamana na Ikulu lakini hakuna hatua yoyote ya
makusudi inayochukuliwa na viongozi wetu na linapopelekwa kwa viongozi
wa kisiasa wanadai waachwe kwani ndio wapiga kura wao" alisema
Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said.
Said alisema katika soko hilo kuna
changoto nyingi za udhalilishaji wanawake kwa kushikwa katika maungo yao
lakini kupitia EfG wamejitahidi kupunguza changamoto hizo kwani
wasaidizi wa sheria waliopatiwa mafunzo na shirika hilo wanajitahidi
kuupenyeza ujuzi waliopata kuifikishia jamii ambayo imeanza kuelewa
kuhusu vitendo hivyo.
Aliongeza kuwa uvaaji wa nguo za kubana
na kuacha vifua wazi kwa upande wa wanawake pia ulikuwa ukichochea
kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji uliokuwa ukifanywa na vijana
wasio rasmi katika eneo hilo la Feri ambao hawana makazi na maisha yao
yapo Feri lakini baada ya kufikiwa na mafunzo ya EfG hali hiyo imepungua
kwa asilimia 80.
Mwezeshaji Fatuma Saijali alisema
changamoto kubwa iliyopo hivi sasa katika soko hilo ni kuzuiliwa kupika
chakula katika eneo hilo la Feri lakini wakati huo huo kuna kundi la
wanawake wamekuwa wakiingiza chakula kutoka majumbano kwao na kukiuza
hivyo kuharibu soko lao la chakula.
Mwenyekiti wa Kamati ya Soko hilo, Ali
Kibwana alisema mafunzo waliyopata kupitia EfG yamesaidia sana kupunguza
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika soko hilo na kila mtu
anayebainika kujihusisha na vitendo hivyo amekuwa akiitwa na kukanywa na
kama akiendelea kuwa mkaidi anachukuliwa hatua nyingine kwa kufuata
kanuni na sheria.
Kamanda wa Ulinzi na Mazingira wa Soko
hilo, Nurdin Hassan amesema hali katika soko hilo ni nzuri kutokana na
kazi kubwa iliyofanywa na EfG ya kufanya semina na matamasha ya
uhamasishaji hivyo kuifanyajamii kuelewa kuhusu vitendo vya ukatili na
udhalilishaji wa kijinsia.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa EfG,
Shaban Rulimbiye alisema Shirika hilo linaendesha mradi wa miaka mitatu
wa Mpe Riziki si Matusi wenye lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili wa
vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji na nia zaidi mradi huo
ni kuusambaza hadi katika maeneo mengine ya nchi.
Tags
HABARI KITAIFA