……………………………………………………………………………………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na uongozi
wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT) ambapo amezungumzia
dhamira ya serikali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali
yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa
Rais aliueleza ujumbe huo kuwa wakati wa kampeni aliahidi pamoja na kazi
za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama atafuatilia kwa karibu
utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na salama, kuboresha
afya ya mama na mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa kwenye kampeni
nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata tabu ya kutembea
mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja na kazi zangu za kumsaidia
Mhe. Rais nitasimamia miradi yote ya maji, alau tuhakikishe maji
yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi wanakoishi au
karibu zaidi”.
Alisema kinachofurahisha zaidi
suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi
mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu katika mikoa kama vile ya
Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi ni kusimamia fedha
zinatumika kuleta maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu afya ya mama na mtoto
alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa kushirikiana na Mashirika
yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za wanawake ili kupunguza vifo
vinavyosababishwa na mimba za utotoni.
“Hili tutajitahidi kulipunguza kwa
kiasi kikubwa na hasa baada ya serikali ya Awamu ya Nne kusema kwamba
shule ya msingi ya lazima ni kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha
nne”, alisema na kuongeza
“Katika kipindi hicho binti
atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa tayari kukabiliana na mambo ya
uzazi tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza darasa la akiwa mdogo na
matokeo yake anapata mimba katika umri mdogo. Mtusaidie kupiga debe huko
nje utekelezaji uweze kufanikiwa.”
Hata hivyo, alisisitiza kusimamia
suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini
zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika wodi za wazazi kwa
ajili ya kuhudumia akina mama na wananchi kwa ujumla ambao wengi
wanaonekana ni watiifu kwa serikali yao.
Kwa upande wa elimu Mhe. Samia
alisema atasimamia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha
mazingira yanatunzwa kwa sababu uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa
chanzo cha upungufu wa maji nchini.
Aidha aliuambia ujumbe huo kuwa
hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali
kuu hadi serikali za mitaa ili kinachopatikana kidogo kimfikie kila
mwananchi.
“Tutaendelea kuaihirisha sherehe
ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya kijamii. Kwa msimamo huu
amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu wote tushirikiane kwa kutatua
matatizo yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi mkubwa.”
Mapema akizungumza kwa niaba ya
wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo Prof Ruth Meena alimpongeza Mhe. Samia
kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka
historia katika Tanzania.
Alimweleza Mhe. Makamu wa Rais
matarajio yao kwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa itatetea misingi ya
haki na usawa katika Nyanja zote.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Tags
HABARI KITAIFA


