Mgombea wa chama cha upinzani cha
Conservative Mauricio Macri amethibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa
urais Argentina, huku mgombea wa chama tawala akikubali kushindwa.
Baada ya karibu kura zote kuhesabiwa, Bw Macri alikuwa na 52% akilinganishwa na Daniel Scioli aliyepata 48%.
Shangwe
na vigelegele vilitanda katika makao makuu ya kampeni ya Bw Macri baada
ya kura za maoni runingani kuonyesha alikuwa ameshinda.
Bw Macri,
meya wa zamani wa Buenos Aires, alikuwa ameshindwa na Scioli, ambaye ni
gavana wa mkoa wa Buenos Aires, kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi
Oktoba.
Lakini wote wawili hawakuweza kushinda moja kwa moja na
duru ya pili ikaandaliwa, mara ya kwanza kwa uchaguzi kuingia duru ya
pili katika historia ya Argentina.
Ushindi wa Bw Macri ndio wa kwanza katika zaidi ya mwongo mmoja kwa upinzani wenye kuegemea siasa za mrengo wa kati kulia.
Aliingia
kwenye uchaguzi huo wa Jumapili akiwa mbele kwa kura za maoni na
alikuwa ameahidi kusisimua uwekezaji na kukabili changamoto za kiuchumi,
uhalifu na ufisadi.
Bw Macri ni mwana wa mmoja wa watu tajiri
zaidi Argentina na alifanya kazi kwa muda mrefu kama mwanabiashara kabla
ya kujitosa katika siasa. |