BANDA MEDIA BLOG

MIILI YA WALIOKUFA MAJI AKIWEMO MSAIDIZI WA IGP YAAGWA KATIKA MJI MDOGO WA KIBAIGWA WILAYANI KONGWA DODOMA

 masanduku ya miili ya marehemu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko Kibaigwa kabla ya kuagwa wilayani Kongwa Dodoma mapema leo Jan 5,2016


BANDA BLOG, Kibaigwa.
MAELFU ya wakazi wa Manispaa ya Dodoma Watumishi wa jeshi la polisi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa jana aliwaongoza  kuaga miili ya marehemu wanne wa familia moja akiwemo msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Gerald Ryoba.


Ryoba akiwa na familia yake akiwemo dereva wake na mfanyakazi wake wa ndani walifariki katika ajali ya gari mjini Kibaigwa baada ya gari lao kusombwa na maji katika eneo la Bwawani.

Akizungumza wakati wa kuiaga miili hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Mkuu huyo wa Mkoa alisema vifo hivyo vimeushtua  uongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla kwani kupoteza familia yote kwa wakati mmoja si jambo la kawaida.

Gallawa aliwataka Wananchi na Wafanyakazi wa Jeshi la Polisi wanatakiwa kuwa watulivu katika kipindi hichi kigumu huku akiwataka kuwaomba kwa Mwenyezimu ili awapokee kwa amani.

 ‘’Niwape pole wafanyakazi wa Jeshi la Polisi pamoja na Watanzania kwa kuondokewa na hawa ndugu zetu,tunatakiwa kuwaombea ili mungu awapokee kwa amani’’alisema Gallawa kwa majonzi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoani hapa,David Misime alisema mara baada ya kuiga miili hiyo Ryoba na familia yake watasafirishwa kuelekea Mkoani Geita.

Kamanda Misime alisema Koplo Ramadhan atasafirishwa kwenda Lindi huku Sara akipelekwa kwao Mbinga Mkoani Ruvuma kwa ajili ya mazishi.

‘’Mara baada ya kumaliza kuaga tutaisafirisha miili kulingana na mahali inapotoka’’alisema

Kwa mujibu wa kamanda huyo alisema juzi Ryoba na familia yake walikuwa wakitokea mkoani Geita kuelekea Dar es salaam kwenye gari lenye namba za usajili T 516 DEP aina ya RAV 4 ilokuwa na jumla ya abiria sita.

Alisema marehemu waliokuwepo katika gari hilo kuwa ni Gerald Ryoba ambaye ni msaidizi wa Mkuu wa jeshi la Polisi nchini, watoto ambao ni Gabriel Gerald Ryoba, Godwin Gerald Ryoba na mkewe Fidea John Kiondo.

Wengine ni Dereva wa gari hilo  F.3243 Koplo Ramadhan, Msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara mwenyeji wa mbinga Mkoani Ruvuma.

Akifafanua kuhusu tukio hilo, Misime alisema  tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tatu usiku katika eneo la kibaigwa linalojulikana kwa jina la bwawani wilayani Kongwa.

Alisema polisi walipata taarifa kuwa kuna maji mengi yanapita katika eneo hilo na yamesababisha magari kushindwa kupita.

Alisema maji hayo yalikuwa yakitiririka  kutoka maeneo ya Njoge na Hembahemba na baada ya kufika eneo la tukio walipata taarifa kuwa kuna gari imesombwa na maji hayo.

 “Lakini baadaye tulipokea taarifa kuwa kuna gari imesombwa na maji lakini inaonekana matairi yapo juu, tulianza kufuatilia na tukazuia magari kuanza kupita na baada ya maji kupungua ndio tukaruhusu magari kupita,”alisema Misime

Aidha alibainisha walianza hekaheka za kutafuta gari hilo na baadaye usiku wa manane walifanikiwa kuipata na baada ya kuitoa kwenye maji walikuta miili ya watu wawili.

“Baada ya kukata lile gari maana lilikuwa limepondeka tukafanikiwa kutoa mwili wa Fidea John Kiondo ambaye ni mwalimu wa manispaa ya Temeke ambaye ni mke wa mkaguzi wa polisi Gerald Ryoba ambaye ni msaidizi wa Afande IGP,”alisema Kamanda huyo.

Hata hivyo alisema walipata taarifa kuwa katika gari hilo kulikuwa na watu sita na ndipo wakaendelea na harakati za kutafuta miili mingine.

“Baadae tulifanikiwa kupata mwili wa dereva wa gari hilo ambaye ni  F.3243 Koplo Ramadhan ambaye naye alifariki na tukaendelea kutafuta na baadaye tukapata mtoto wa miaka minne Gabriel Gerald Ryoba na hatimaye tukapata mwili wa Godwin Gerald Ryoba,”alisema Misime.

Hata hivyo alisema Mwili wa Mkaguzi huyo ulipatikana jana saa 10:20 asubuhi na pia katika gari hilo kulikuwa na Msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara.
mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG