Naibu Waziri wa Afya Ustawi wa
Jamii Jinsia Watoto na Wazee Dk Khamis Kigwangala akizungumza na
waandishi wa habari wakati alipotoa tamko la wizara hiyo kuhusu
kipindupindu kwenye mkutano uliofanyika wizarani hapo leo ukihudhuriwa
na wataalam mbalimbali wa afya kutoka wizara hiyo.
Dk. Rufaro Chatora Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Afya Duniani WHO akizungumza jambo katika mkutano
huo kushoto ni Naibu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Watoto na
Wazee Dk Khamis Kigwangala akimsikiliza kwa makini.
Ninapenda kutoa taarifa kwa umma,
kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu ulioanza tarehe 15 Agosti,
2015 katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa kwa kasi katika Mikoa
mingine 21 ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani, Morogoro, Iringa,
Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita, Mara, Manyara, Arusha, Shinyanga,
Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Kagera, Katavi, Mbeya na Mwanza na
Simiyu.
Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya
watu 12,810 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 202
wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya
waliougua. Katika kipindi cha wiki iliyoanza tarehe 28 Desemba 2015 hadi
tarehe 3 Januari 2016, kumekuwa na jumla ya wagonjwa walioripotiwa 590
na vifo 6, ambayo ni asilimia 0.01 ya wagonjwa wote. Mkoa wa Mara
(Musoma Mjini) ndio ulikuwa unaongoza kwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa
wa kipindupindu ukifuatiwa na Singida (Iramba), Morogoro (Morogoro
Vijijini) na Manyara (Simanjiro).
Takwimu zinaonyesha kuwa licha ya
kuwa na nafuu katika wiki ya nyuma, wiki hii kasi ya maambukizi
inaonesha kupanda tena kwenye mikoa ya Mwanza na Arusha. Katika mkoa wa
Arusha, maambukizi yamepanda kutoka wagonjwa wapya 60 hadi 111 kwa
wiki. Katika mkoa wa Mwanza, kasi ya maambukizi imepanda kutoka
wagonjwa wapya 45 hadi 66 kwa wiki.
Kasi ya maambukizi ya
Kipindupindu katika wiki iliyopita imepungua kwa kiasi kikubwa katika
mikoa ya Mbeya na Tanga. Aidha, mikoa ya Dar-es-Salaam na Lindi
haijaripoti mgonjwa yeyote mpya wa Kipindupindu katika wiki iliyopita.
Tunawapongeza kwa hatua hii kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau
ambao kwa pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa karibu zaidi.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Sekta nyingine
husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea kukabiliana na
ugonjwa huu kwa njia mbalimbali. Kikosi kazi maalum chini ya uratibu wa
Ofisi ya Waziri Mkuu kinakamilisha mpango unaoshirikisha Wizara ya Afya
Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto , TAMISEMI, Wizara ya Maji
na Umwagiliaji, DAWASCO, DAWASA, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi pamoja na Sekretariat ya Mkoa wa Dar-es-Salaam, kwa ajili ya
kuhakikisha kuwa mikakati ya kupambana na ugonjwa huu inakuwa jumuishi
na ya haraka.
Bado Wizara inaendelea kusisitiza
kuwa, ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa
huu, wananchi wanasisitizwa kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka
kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama,
kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka:-
- Kabla na baada ya kula
- Baada ya kutoka chooni
- Baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
- Baada ya kumhudumia mgonjwa
Aidha, ni muhimu kuhakikisha kuwa
wananchi wanatumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika
vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani. Wizara ilishapiga marufuku
kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula barabarani katika mazingira yasiyo
safi na salama. Hivyo, Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na
watendaji ambao ni Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya,
ziendelee kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa jambo hili.
Wizara inapeleka tena timu za
wataalm katika mikoa iliyoathirika zaidi na kipindupindu ambayo ni
Simiyu, Mara, Morogoro, Manyara, Singida, Arusha na Mwanza. Timu hizi
zitaungana na timu za mkoa wa wilaya kusaidia kudhibiti ugonjwa huu.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kukumbusha kuwa, mikoa ambayo
bado haijaathirika ichukue hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate
mgonjwa yeyote wa Kipindupindu.
Tags
AFYA