Timu ya Acacia Stand
United fc (CHAMA LA WANA) imejidhatiti vilivyo kuelekea mchezo wake wa
kesho wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Maafande wa jeshi la
kujenga taifa JKT Ruvu kutoka Pwani.
Afisa habari wa “CHAMA LA
WANA”ISAAC EDWARD amesema wako vizuri kuwaangamiza maafande hao na kuzoa
pointi zote tatu ili kuwapa furaha mashabiki wao ambayo waliikosa
katika mchezo wao uliopita walipofungwa nyumbani dhidi ya Simba sc.
“kiukweli tumejidhatiti vilivyo
kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya JKT Ruvu,tuna kila sababu ya
kushinda mchezo huo licha ya kuwa maafande hao wana kikosi kizuri na
benchi la ufundi lenye watu wazoefu na soka la Tanzania lakini haitakuwa
sababu ya kushindwa kuwapa kichapo”
Edward ameongeza kuwa kikosi chao
kinazidi kuimalika kila kukicha na pia ujio wa wachezaji wao Haruna
Chanongo na Abuu Ubwa kambini umeongeza Morali kambini.
“hali ya kikosi hivi sasa iko
vizuri na Morali kwa wachezaji ni ya juu sana ukizingatia Haruna
Chanongo na Abuu Ubwa wamejumuika na kikosi kambini toka siku ya
jumatatu na wameendelea na Programu za mwalimu kama kawaida,Hapana shaka
panapo majaaliwa yake mwenyezi mungu na kutokana na mfumo wa mwalimu
Patrick Liewing na mahitaji yake basi siku ya kesho watashuka dimbani
kuisaidia timu”
Pia amewaomba mashabiki na
wapenzi wa klabu hiyo pendwa mkoani shinyanga kujitokeza kwa wingi
kuishangilia kwani katika kipindi hiki cha mzunguko wa pili wa ligi,timu
inahitaji sana kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwao ili ifanye vizuri
katika michezo yake ijayo na hatimae kushika nafasi za juu pindi ligi
itakapo fikia tamati.
“nawaomba mashabiki na wapenzi wa
Acacia Stand United Fc kujitokeza kwa wingi siku ya kesho katika uwanja
wa kambarage kuishangilia timu yao ili iweze kupata matokeo mazuri ya
ushindi ili tuweze kukaa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi na
hasa katika kipindi hiki cha mzunguko wa pili wa ligi timu inahitaji
sana sapoti ya mashabiki tufanikishe kushinda mechi zilizobaki na
hatimae mwisho wa ligi tukae katika nafasi za juu”
Acacia Stand United Fc kesho
inashuka dimbani katika uwanja wake wa nyumbani CCM Kambarage mjini
shinyanga kucheza na JKT Ruvu ikiwa ni muendelezo wa michezo ya ligi kuu
ya Vodacom Tanzania Bara.
Tags
MICHEZO KITAIFA