Anitha Jonas – MAELEZO
TANGU enzi za Azimio la Arusha,
suala la maadili limekuwa likisisitizwa kama nguzo muhimu katika utoaji
wa huduma kwa umma. Lengo lilikuwa ni kuhakakisha kwamba kila mtumishi
wa Umma anatekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo
iliyowekwa.
Kutofanikiwa kwa Azimio la
Arusha kulitokana na baadhi ya Viongozi kujua kwamba utekelezaji wa
malengo ya azimio hilo ungekwamisha nia ovu waliyokuwanayo kama
Watumishi wa Umma katika kuwahudumia Wananchi. Ndio maana juhudi ya
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kutaka azimio
hilo liungwe mkono hazikuzaa matunda.
Pamoja na kuwepo sheria,
kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili kwa watumishi wa Sekta ya
Umma na watu binafsi, wananchi bado wamekuwa wakilalamika kuwepo
urasimu usio wa lazima wenye lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa na
huduma zisizoridhisha. Aidha, wapo baadhi ya wafanyabishara binafsi
wasiozingatia maadili na hata kufikia hatua ya kuchochea utoaji wa
rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na viwango.
Katika jitihada za kuhakikisha
kwamba watumishi wa Umma wanakuwa waadilifu na wanafuata maadili mema,
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete
ilibuni mikakati ya kuwa na utaratibu mpya kwa viongozi na watumishi wa
Sekta za Umma na Binafsi kusaini Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge).
Ahadi ya Uadilifu ni tamko
rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na mwenendo wa kimaadili na kuunga
mkono kampeni ya kitaifa ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa. Kwa
kusaini tamko hilo, mhusika au taasisi inakuwa imejipambanua kwa Umma
kuwa haitajiingiza katika masuala yasiyo ya kimaadili katika utoaji
huduma na uendeshaji wa biashara.
Kwa mujibu wa Kamishina wa
Maadili Jaji Salome Kaganda, kuna aina tatu za hati za Ahadi ya Uadilifu
yaani; Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, Watumishi wa Umma na
Sekta binafsi ili kila kundi liwajibike kwa namna yake.
Akizindua Hati za Uadilifu
mwezi agosti 2015, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema, kuwepo kwa Hati
hizo ni hatua kubwa muhimu na ya kihistoria katika safari ya kuboresha
na kuhuisha mifumo ya uadilifu iliyopo ili iweze kwenda sambamba na
mazingira na nyakati zilizopo.
Tags
HABARI KITAIFA