……………………………………………………………………………………………………………………….
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli
amekabidhi chakula kwa ajili ya futari wakati huu wa mfungo wa mwezi
Mtukufu wa Ramadhani kwa vituo vinne vya kulea watoto yatima na wale
waishio katika mazingira magumu Jijini Dar es salaam.
Vyakula hivyo vimekabidhiwa leo
tarehe 18 Juni, 2016 katika ofisi ya Mke wa Rais Ikulu Jijini Dar es
salaam vimejumuisha Mchele kilogramu 500, Sukari kilogram 500 na Tende
kilogramu 28.
Akizungumza mara baada ya
kukabidhi vyakula hivyo, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli aliyeongozana
na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewatakia heri Waislamu wote
katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasihi waendelee
kuliombea Taifa amani na utulivu.
(“Tunawatakia mfungo mwema
wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, katika kipindi hiki tunawaomba mzidi
kuiombea nchi yetu amani, viongozi wetu wa nchi na watanzania wote kwa
ujumla, nchi ikiwa na amani ndio mambo mengi mazuri yanaweza kufanyika”)
Kwa niaba ya vituo vilivyopatiwa
vyakula hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Charambe Islamic Center Dkt.
Haruni Kondo amemshukuru Mke wa Rais kwa kutoa vyakula hivyo na ameeleza
kuwa kitendo hicho kinaonesha mshikamano na ushirikiano walionao
watanzania wote bila kujali tofauti ya dini, kabila wala maeneo
wanayotoka.
(“Kwa hiyo ndugu zangu mna
imani ya kikristo lakini mnatambua waislamu ni ndugu zenu, wote
tunajenga nyumba moja, mshikamano ndio tunu tuliyoachiwa na Baba yetu wa
Taifa, leo mmeguswa kuona wenzenu tunafanya ibada na nyinyi mmeingia
kwenye ibada, sasa ibada ya kutoa ni ibada kubwa sana, sio nchi nyingi
katika Afrika zinafanya kitendo hiki, watu hawaelewi, ni nchi chache
sana ambazo imani moja inaunga mkono imani nyingine, lakini sisi
waislamu tunalitambua hili hata toka kipindi ambacho mtume wetu SWA
anapigana kusimika dini hii kwa waumini alipata nusura kwa wakristo”)
Vituo vilivyokabidhiwa vyakula hivyo ni Charambe Islamic Center, Tasofe Lqadiria, Nur Twarigatu Lqadiria na Zawiyatul Lqadiria.
Tags
HABARI KITAIFA