BANDA MEDIA BLOG

NIONAVYO MIMI: CONTE MAN OF THE MATCH ITALY VS BELGIUM, MBINU ZAKE ZILIWAVURUGA HAZARD NA NDUGUZE

Conte
Hadi sasa ushindi mnono kwenye mashindano ya Euro ni wa mabao 2-0, mabingwa mara 4 wa kombe la dunia Italy pamoja na Ujerumani ndiyo timu pekee ambazo zimepata ushindi huo dhidi ya mataifa ya Belgium na Ukraine.
Anyways wacha nirejee kwenye mchezo wa jana usiku (Belgium vs Italy) ufundi wa kimbinu wa hali ya juu kutoka kwa Antonio Conte ulisaidia kuwafanya wachezaji wakali wa Belgium waonekane wa kawaida, mfumo 3:3:4 ulikilazimisha kikosi cha Marc Wilmots kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mabeki wawili wa pembeni wa Azzuri (Matteo Damian & Antonio Candreva) muda mwingi walikuwa wanatanua na kushambulia kupitia pembeni kitu ambacho kiliwalazimu viungo wa Belgium (Witsel & Naiggolan) nao kulazimika kwenda pembeni na kuacha nafasi kubwa katikati iliyokuwa inatumiwa vizuri na Italy kufanya build up ya mashambulizi.
Iliwalazimu mawinga wa Belgium Hazard pamoja na De Bruyne kwa muda mwingi kurudi nyuma kuwakaba walinzi wa pembeni wa Italy Damian na Candreva kosa jingine kubwa kwenye kikosi cha Belgium ni kitendo cha kuwatumia mabeki wote wenye asili ya kucheza kati kwenye mchezo mmoja.
‘Kocha akiandaa mfumo mzuri basi mfumo huo hupelekea kuwafanya wachezaji wakali wa timu pinzani kuwa wa kawaida’. Jana man of the match alikuwa Antonio Conte.

Mbinu za Conte zilivyoivuruga Belgium  
Kabla ya michuano hii kuanza wachambuzi walianza kukiponda kikosi cha Italy kwamba hakina ubora lakini kocha wa timu hiyo Antonio Conte alisema: “Sio muda muafaka kwa soka letu.”
Kocha huyo ambaye baada ya michuano hii ataelekea pale darajani jijini London aliongeza kwa kusema: “Muhimu ni kwamba, kikosi kina ari. Nimefanya kazi kubwa juu ya hilo.”
Ushahidi katika mchezo wa jana si ari pakeyake iliyowapa matokeo waliyoyahitaji Italy. Bali utaona namna ambavyo kikosi kilivyokuwa na mpangilio na nidhamu ya mchezo ya hali ya juu dhidi ya wachezaji wa Belgium wenye majina makubwa kwa mchezaji mmoja-mmoja ambao walimiliki mpira kwa asilimia nyingi ukilinganisha na wale wazee wa The Azzurri
Timu 16 kati ya 24 ndiyo zitasonga mbele baada ya hatua ya makundi kumalizika, Italy wameshajiweka mahali pazuri mara baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza dhidi ya wapinzani wao wakubwa kwenye Kundi E.
Hawa jamaa wametwaa taji hili mara moja tu mwaka 1968 huku wakimaliza kama washindi wa pili mara mbili lakini 2012 ndiyo inakumbukwa zaidi kwa sababu ndiyo mara yao ya mwisho kumaliza katika nafasi ya pili katika miaka ya hivi karibuni walipokubali kichapo cha bao 4-0 kytoka kwa Spain kwenye mchezo wa fainali.
Ikumbukwe kikosi cha Italy hakijapoteza mechi wakai wa kuwania kufuzu michuano ya Euro 2016, kikiwa kimeshinda mechi saba kati ya 10 wanafananishwa na kikosi kile cha miaka minne iliyopita ambacho hakikupewa nafasi ya kufanya lolote kwenye michuano hiyo. Wakikosa huduma ya fundi mkongwe na m-bunifu Andrea Pirlo kwenye eneo la katikati pamoja na striker wao aliyeporomoka kiwango Mario Balotelli, Italy wanabebwa na mbinu kali za Conte zinazotekelezwa vema uwanjani pamoja na ukuta mgumu unaoundwa na mabeki wa Juventus.
Wakiwa wamefuzu michuano hiyo mikubwa barani Ulaya baada ya miaka 14 iliyopita, Belgium wamekuja ufaranza wakiwa timu inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ndoo pale Paris Julai 10.
Timu yao inajengwa na wachezaji wenye majina makubwa wanaovitumikia vilabu vyenye majina barani Ulaya kama Kevin de Bruyne, Eden Hazard na Lukaku lakini hawa wote walishindwa kuonesha ubora wao wakiwa na timu ya taifa na kushindwa kutamba mbele ya waitaliano 11 walio chini ya Conte.
Walikuwa wakiishia kukimbia muda mwingi wa kipindi cha kwanza, wakishindwa kupenya nyuma ya ukuta wa Italy huku De Bruyne akionekana kuwa na uhai zaidi ukilinganisha na wachezaji wengine.
Wakaongeza speed ya mchezo baada ya kutoka mapumziko lakini bado hawakuweza kuzifungua nyavu zilizokuwa chini ya ulinzi mkali wa Gianluigi Buffon. Lukaku akapoteza nafasi muhimu alipou-chop mpira ukatoka centimeter chache golini kabla ya kupumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Origi ambaye pia mipira yake miwili ya kichwa ilikosa macho.
Jambo ambalo pia nimeliona kama udhaifu mwingine wa Belgium ni safu yao ya ulinzi, kukosekana kwa Vincent Kompany kulichangia kwa kiasi fulani kukosa umakini kwa walinzi wa Belgium lakini kumchezesha Jan Vertonghen kama mlinzi wa pembeni bala ya katikati pamoja na mchezaji mwenzake Toby Alderweireld kama wanavyocheza Tottenham lilikuwa ni kosa jingine.
Timu zote zitakuwa na vibarua dhidi ya Jamhuri ya Ireland na Sweden ambazo zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi E.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG