Picha na mpiga picha wetu
…………………………………………………………………………………………………..
Na Benny Mwaipaja, WFM
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa Tanzania imejipanga
kuimarisha mapato yake ya ndani ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Pili
wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.
Dkt. Likwelile, amesema hayo
Mjini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku 2 unaowahusisha
wataalamu wa Uchumi na Mipango wapatao 170 kutoka nchi nzima.
Amesema kuwa misaada kutoka kwa
wadau wa maendeleo imekuwa ikipungua kila wakati, hatua ambayo imeifanya
Serikali kuendelea kujipanga kukabiliana na nakisi ya Bajeti yake ili
kukuza maendeleo.
“Mikopo yenye riba nafuu nayo
imepungua, sasa hivi unaenda kukopa kibiashara, kwa uchumi wetu huu
hatuwezi kumudu” alisisitiza Dkt. Likwelile
Ameeleza kuwa Tanzania
inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuimarisha miundombinu ya barabara,
reli, bandari na mambo mengine, hali inayohitaji fedha nyingi ambazo
zitapatika kwa kukusanya kodi mbalimbali.
Amewataka wataalamu hao wa uchumi
na mipango kujadili na kuibuka na mipango itakayosaidia kufanikisha
utekelezaji wa Mpango huo wa Pili wa Maendeleo wa Taifa unaotarajiwa
kugharimu shilingi Trilioni 107.
Akifungua mkutano huo kwa niaba
ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wataalamu hao kutoa mapendekezo
ya kitaalamu wakizingatia changamoto mbalimbali zikiwemo za kupanda kwa
gharama za mafuta duniani.
Vilevile, amewakumbusha umuhimu
wa kutumia takwimu sahihi wakati wa kupanga namna bora ya kutekeleza
mpango huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na watanazania kuwaletea
maendeleo ya haraka
“Takwimu ndizo zinazotoa picha
halisi ya matatizo yanayowakabili watanzania ukiwemo umasikini, ambapo
zikitumika vizuri zitasaidia kupanga namna bora ya wananchi wanavyoweza
kuondokana na umasikini huo” Alisisitiza Dkt. Mwakyembe
Kwa upande wake, Kaimu Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri, amesema kuwa Tanzania
imedhamiria kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka
2025.
Amesema kuwa hatua hiyo itafikiwa
kwa kuelekeza nguvu kubwa katika uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda
kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwanri amesema kuwa hatua hiyo
itakuza uchumi wa nchi kwa kuongeza kipato cha wananchi pamoja na ajira
na akasisitiza umuhimu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujitolea
utaalamu na nguvu zao zote kufanikisha malengo hayo.
Tags
HABARI KITAIFA