BANDA MEDIA BLOG

USHINDI WA KWANZA BAADA YA MIAKA 18 CAF, NA SABABU NYINGINE ZA KUANGUKA KWA YANGA

IMG_0007
Na Baraka Mbolembole
USHINDI wa 1-0 dhidi ya MO Bejaia haujatosha kwa mabingwa wa Tanzania Bara, timu ya Yanga SC kuwapeleka nusu fainali katika Caf Confederation Cup 2016 lakini una maana kubwa sana kwa timu hiyo baada ya kusubiri kwa michezo kumi ya hatua ya makundi pasipo kupata ushindi.
Huu ni mpango ‘B’ ambao nilisema Yanga wanapaswa kuhakikisha wanautimiza mara baada ya kufungwa 3-1 na Medeama SC wiki mbili zilizopita.

Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Bara sasa wataenda Lubumbashi baadae mwezi huu kukamilisha tu ratiba ya michuano hiyo katika kundi A kwani tayari wametupwa nje ya michuano kufuatia TP Mazembe kulazwa 3-2 na Medeama siku ya jana Jumapili.
Msimamo wa Kundi A
TP tayari wamefuzu kwa nusu fainali baada ya kukusanya pointi 10 katika michezo yao mitano. Medeama wanafuatia kwa karibu wakiwa na alama 8. Bejaia wamebaki na pointi zao tano huku mabingwa wa VPL wakiwa na alama nne.
Kila timu imebakiwa na game moja (Mazembe v Yanga, Bejaia v Medeama). Kwa maana hiyo vita ya timu ya pili itakayofuzu kwa nusu fainali imebaki kwa timu mbili, Bejaia kutoka Algeria na Medeama ya Ghana.
Mazembe watalazimika kuifunga Yanga katika game ya mwisho ili kumaliza kama vinara wa kundi, japokuwa wanaweza pia kubaki kileleni ikiwa Medeama watashindwa kupata ushindi katika game yao ya mwisho.
Uwanja wa taifa umewaangusha Yanga
Bila shaka kikosi cha Hans Van der Pluijm kitakuwa kinakumbuka namna kilivyokubali kuangusha pointi muhimu katika uwanja wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe ambao waliifunga Yanga 1-0 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia, sare ya kusikitisha (1-1) dhidi ya Medeama ilimaanisha kuwa, Yanga iliangusha pointi nne muhimu ambazo zingewafanya kuwa na alama 8 katika kundi kama wangepata ushindi.
Mazembe na Medeama hadi sasa zimenufaika na viwanja vyao vya nyumbani kwa kuwa wamefanikiwa kukusanya pointi za kutosha.
Medeama imepata alama 7 katika uwanja wake wa nyumbani (Medeama 0-0 Bejaia, Medeama 3-1 Yanga, Medeama 3-2 Mazembe).  Ni pointi moja tu wamefanikiwa kuipata katika uwanja wa ugenini walipokuja Dar na kulazimisha sare ya kufungana 1-1 na Yanga.
Mazembe hawajaangusha pointi yoyote katika uwanja wao wa nyumbani (Mazembe 3-1 Medeama, Mazembe 2-0 Bejaia). Ukitazama namna soka la Afrika linavyochezwa ili ufanikiwe ni lazima kwanza uwe na uwezo wa kupata matokeo katika uwanja wa nyumbani.
Yanga walipaswa kuifunga Medeama katika uwanja wa Taifa na kupata sare au ushindi dhidi ya Mazembe lakini kitendo cha kushindwa kufanya hivyo kimewaondoa katika michuano.
Kushindwa kupata sare ugenini
Unapocheza michuano yenye game tatu za nyumbani na tatu za ugenini, ni lazima uhakikishe unapata alama zisizopungua 7 katika uwanja wa nyumbani na matokeo ya sare ugenini yanamaanisha una mzuia mpinzani kukupita au kukukaribia.
Kufungwa ni sawa na kutoa nafasi ya mpinzani kukuacha kwa umbali. Yanga imeshindwa kupata hata sare moja ugenini (Bejaia 1-0 Yanga, Medeama 3-1 Yanga).
Ni tofauti na Mazembe na Medeama ambao wamefanikiwa kupata sare moja ugenini sawa na Bejaia. Kushindwa kupata matokeo ugenini pia kumewaangusha sana wawakilishi hao wa Tanzania.
Wakiwa tayari na tiketi ya CAF Champions League 2017, Yanga wanapaswa kuuchukulia ushindi wao wa kwanza katika hatua ya makundi kama mwongozo wa kupiga hatua zaidi, huku wakijifunza zaidi namna ya kusaka ushindi katika uwanja wa nyumbani. Katika soka la Afrika ukishindwa kupata matokeo nyumbani utaishia kuwa msindikizaji tu.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG