Na Baraka Mbolembole
PASS ACADEMY ‘Player Academy For Skills and Strategy’ ni academy ya soka inayomilikiwa na Mtanzania, Alex Kajumulo. Makao yake makuu ni Seattle, Washington, Marekani.
“Miaka 15 iliyopita ndiyo nilianzisha academy hii kwa sasa kuna vijana 1000. Wote ni vijana wa hapa Marekani” anasema Kajumulo nilipofanya naye mahojiano marefu akiwa US.
Kajumulo amewahi kumiliki timu ya soka hapa nchini mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 tayari amefungua tawi la PASS ACADEMY nchini Uingereza na sasa yupo katika hatua za mwisho kuanzisha ligi yake mwenyewe.
Unaweza kujiuliza ni namna gani Mtanzania huyo anaweza kuwamiliki vijana 1000.
“Kila mtoto analipa dolla 3000 kwa mwaka. Nina timu za watoto wadogo na za wakubwa na hivi sasa ninaanzisha ligi yangu mwenyewe ambayo itafahamika kama 2016 Washington Soccer Association Youth Premier League. Sheria zinaruhusu kuanzisha ligi yangu mwenyewe”, anaendelea kusema mmiliki huyo wa zamani wa timu ya Kajumulo World Soccer.
Kwa vijana 1000 alio nao katika academy yake na kiasi cha ada wanazolipa kwa mwaka, Kajumulo atakuwa akiingiza dolla milioni 3 kwa mwaka. Nilimuuliza kama ana mpango wa kuja kuwekeza hapa nyumbani Tanzania.
“Ndio, nitakuja kuwekeza pia nyumbani lakini kwa sasa nitaanza na Bukoba. Nategemea kuja huko mwezi Desemba kwa ajili ya mpango huo”, anasema, Kajumulo ambaye academy zake za US na UK zina mkusanyiko wa vijana wa kiume (wavulana) na wale wa jinsia ya kike (wasichana.)
“Kuna wavulana wapatao 600 na wasichana 400 katika academy hapa US. Baada ya kucheza hapa watoto huwa wanapata nafasi ya kwenda Univeristy kucheza mpira.”
Tags
MICHEZO KIMATAIFA