Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
Serikali ina uwezo wa kugundua
barabara iiliyojengwa chini ya kiwango kwa kukagua miradi inayotekelezwa
wakati wote wa ujenzi wa miradi hiyo hata baada ya kukamilika kabla ya
muda wa ukaguzi wa mwisho kupita.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani alipokuwa
akijibu swali la Miza Bakari Haji Mbunge wa Viti Maalum lililohoji kama
Serikali inaweza kugundua ni barabara ngapi zilizotengenezwa chini ya
kiwango nchini.
Mhandisi Ngonyani alizitaja
barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami ambazo zilikuwa matatizo
mbalimbali kabla ya muda uliotarajiwa kuwa ni pamoja na Kilwa ambayo
inaanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Bendera Tatu, Sekenke hadi Shelui,
Kyamorwa hadi Buzirayombo na Nangurukuru hadi Mbwemukulu.
Barabara hizo zilipokamilika
yalijitokeza matatizo mbalimbali kabla ya muda uliotarajiwa yanayotokana
na mapungufu kwenye ubora kama mashimo katika barabara hizo na
kuharibika kwa tabaka mbili za juu.
Mhandisi Ngonyani amesema kuwa
ujenzi wa barabara hutengenezwa kwa kuzingatia mikataba kati ya TANROADS
na Mkandarasi na kati ya TANROADS na Mhandisi Msimamizi na viwango
vinavyotakiwa kwenye ujenzi wa mradi huo wa barabara vimetajwa kwenye
mkataba husika.
“Endapo kunatokea tatizo lolote
kuhusu ubora wa kazi, kwa mfano barabara kujengwa chini ya kiwango,
vipengele vya mkataba husika vitatumika kubaini nani aliyesababisha
mapungufu hayo kati ya Mkandarasi, Mhandisi Msimamizi au mwajiri na
hatimaye kuwajibika” alisema Mhandisi Ngonyani.
Katika kudhibiti nidhamu ya
kuheshimu mikataba, Mhandisi Ngonyani alisema kuwa kutokana na mapungufu
yaliyojitokeza katika mradi wa ujenzi wa barabara husika hatua
zilichukuliwa kulingana na vipengele vya mikataba husika na Mkandarasi
wa miradi hiyo walirekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika barabara
hizo kwa gharama zao wenyewe.
Wingi wa magari nao umeainishwa
kuwa ni sababu nyingine ambayo inasababisha uharibifu wa barabara
kutokana na wingi wa magari makubwa ya mizigo yanayotumia ekseli zenye
tairi moja.
Ili kuhakikisha uthibiti wa uzito
wa magari, Serikali inafanya utaratibu wa kufanya mabadiliko ya kanuni
za usalama barabarani za mwaka 2001 ziweze kuoana na Sheria ya Uthibiti
wa uzito wa magari ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambayo imeweka
kiwango cha uzito wa tani 8.5 kwenye ekseli zenye tairi moja.
Akijibu swali la Mbunge wa
Nanyumbu Mhe. Dua William Nkurua aliyehoji ni lini Serikali itatekeleza
miradi ya barabara wilaya ya Nanyumbu, Mhandisi Ngonyani alisema kuwa
Wakala wa Barabara Tanzania imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa
kina wa barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu hatua ambayo itasaidia
kujengwa kwa barabara hiyo.
Tags
Bunge