Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akilihutubia Bunge kabla ya kutoa
kauli ya kuliahirisha bunge hilo mpaka tarehe 1 Novemba 2016 ambapo
mbali na mambo mengine amesema serikali itaendelea kutekeleza yale
iliyoyaahidi na kuwashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujitolea
kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, wakati wa
kikao cha nane cha Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Na Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na
Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
Akihitimisha Bunge, Waziri Mkuu
ameainisha mambo mbalimbali ambayo yamefanyika wakati wa Mkutano huo
ikiwa ni pamoja na mijadala mbalimbali inayohusu miswada ya sheria
iliyosomwa kwa mara ya kwanza, mara pili na kwa mara ya tatu.
Waziri Mkuu amesema kuwa mijadala ya mkutano huo ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga katika kuleta maendeleo nchini.
“Nawapongeza sana wabunge wote
kutokana na michango yenu mizuri na yenye tija hatua ambayo ilibidi mara
kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku ikiwa ni nje ya muda wa kanuni
za Bunge” amesisitiza Waziri Mkuu.
Katika kuhitimisha mkutano huo,
Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya matukio mbalimbali yaliyotokea nchini
ikiwemo janga la tetemeko la ardhi, shughuli za bunge, mwenendo na
mwelekeo wa hali ya uchumi, mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali,
mpango wa Serikali kuhamia Dodoma, hali ya upatikanaji wa chakula
nchini, maboresho katika tasnia ya Ushirika, Sekta ya elimu, suala la
uhakiki wa vyeti kwa watumishi, kuimarisha usafiri wa anga, hali ya
amani na utulivu nchini pamoja na suala la michezo nchini.
Akizungumzia kuhusu janga la
tetemeko la ardhi lililotokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, Waziri Mkuu ametoa
wito kwa wananchi, Sekta binafsi na Jumuiya za Kimataifa kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.
“Serikali inaendelea kukusanya
michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, waliotayari kuchangia
wanaweza kutumia akaunti ya maafa iliyofunguliwa benki ya CRDB yenye
namba 0152225617300 kwa jina la Kamati ya Maafa Kagera na kwa njia ya
simu michango hiyo inaweza kutumwa pia kupitia M-pesa 0768-196669, Airtel Money 0682-950009 na Tigo pesa 0718-069616” amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa upande wa mwenendo na
mwelekeo wa hali ya uchumi nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa ujumla
hali ya uchumi nchini inaridhisha na inaendelea kuimarika.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) hali ya uchumi umeimarika ambapo pato la Taifa lilikua
asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa mwaka 2015, ukuaji huo
unatoka na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano,
utangazaji na huduma za intaneti na kuongezeka kwa uchimbaji wa madini.
Katika suala la ukusanyaji wa
mapato ya Serikali kwa mwezi Julai na Agosti, Waziri Mkuu amesema kuwa
takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho mapato yanayokusanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi Trilioni 2.168
ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113 ikiwa
ni sawa na ongezeko la asilimia 103 ya lengo la Serikali.
Waziri Mkuu amesema kuwa, katika
mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya
tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji
wa Makao Makuu Dodoma ambapo utekelezaji wake utakuwa wa awamu sita.
Vilevile katika sekta ya Kilimo,
Waziri Mkuu amesema kuwa hali uzalishaji na upatikanaji wa chakula
nchini umefika tani 16,172,841, ambapo Serikali imetoa ruzuku za
pembejeo za kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula hususani mahindi,
mpunga na mtama, kwa upande wa mazao ya biashara ruzuku hiyo hutolewa
katoka mazao ya korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti.
Pia Serikali itafanya
marekebisho ndani ya tume ya maendeleo ya Ushirika na kuchukua hatua za
kinidhamu kwa watakao bainika na ubadhirifu wa mali za ushirika.
Katika Sekta ya Elimu, Waziri
Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua walimu wapya watakaoajiriwa
wapangiwe vituo vya kazi moja kwa moja na kwa kuzingatia maeneo yenye
upungufu wa walimu.
Kuhusu uhakiki wa vyeti vya
watumishi, Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la
uhakiki wa vyeti vya watumishi na kuwaagiza wagurugenzi wa halmashauri
kuandaa vituo maalum ambavyo vipo jirani na vituo vya kazi ili
kuwapunguzia watumishi gharama na adha wakati wa zoezi hilo.
Katika kuboresha usafiri wa anga
nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imenunua ndege mbili aina ya
Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zitakazotumika
kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na chi jirani.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema
kuwa vyombo vya usalama na ulinzi nchini vimeendelea kulinda na
kudumisha amani na utulivu nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi ili
kufanikisha lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza
Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kwa kuiwakilisha vyema Tanzania
katika mashindano ya Kimataifa.
Mbali na hayo Waziri Mkuu
Majaliwa amepokea michango mbalimbali iliyotolewa na Kampuni ya Caspian
shilingi milioni 100, Ofisi ya Taifa ya Takwimu shilinhi milioni 1.6 na
kampuni ya Bordar Ltd shilingi milioni 20 kwa ajili ya waadhirika wa
tetemeko lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mikoa ya Kanda
ya Ziwa.
Tags
Bunge