Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi
wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Kulia ni
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Ninatubu Lema.
Wajumbe wa Bodi wakimsikiliza
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(hayupo
pichani), wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi
Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Prof.
Ninatubu Lema (kulia) wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya
.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege (TAA) Prof. Ninatubu Lema, akifafanua jambo kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto),
wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo. Kulia kwake ni MKurugenzi wa
Miundombinu ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng.
Hussein Mativila.
……………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kusimamia Menejimenti ya Mamlaka hiyo
katika Idara ya Utawala na Rasilimali watu ili kuhakikisha ajira zote
zinazotolewa zinazingatia sifa na vigezo vya kuajiri.
Akizungumza katika uzinduzi wa
Bodi hiyo mpya jijini Dar es salaam pamoja na mambo mengine, Profesa
Mbarawa ameisisitiza bodi hiyo kuifanyia kazi Ripoti ya Uchunguzi wa
uendeshaji wa Viwanja hivyo nchini na kufanya mabadiliko mara moja.
“Nataka muipitie ripoti
niliyomkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mkuu na mufanyie maamuzi, suala la
kuajiri watu kiholela, ninataka wote waliandikwa kwenye ripoti hiyo kuwa
hawana sifa watolewe wapishwe watu wenye sifa ili waweze kufanya kazi”,
amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameitaka
Bodi hiyo kusimamia kwa uadilifu miundombinu yote ya viwanja vya ndege
nchini na kuhakikisha mashine za ukaguzi zinafanya kazi masaa 24 ili
kudhibiti mianya yote ya rushwa.
Ameitaka Bodi hiyo kusimamia
vizuri ukusanyaji wa mapato katika viwanja vyote ili kuweza kufikia
lengo lililowekwa na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, Profesa Mbarawa ameitaka
Bodi hiyo kushirikiana na wafanyakazi wa Viwanja hivyo katika mambo
mbalimbali ili kuboresha utendaji na kuweka uwazi katika utoaji wa
huduma katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Bodi hiyo, Profesa Ninatubu Lema amemhakikishia Waziri huyo kuwa
ataongeza ushirikiano na wafanyakazi wote na kusimamia maagizo yote
yaliyotolewa.
Ameahidi kuboresha huduma katika
viwanja vyote nchini na kusema kuwa umuhimu wake utaongeza mapato
katika viwanja hivyo na nchi kwa ujumla.
Tags
HABARI KITAIFA