Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya kufungua Mkutano wa Sita wa
Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Jenista Mhagama na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya kufungua Mkutano wa Sita wa
Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
Oktoba 20, 2016. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisiya Waziri Mkuu,
Jenista Mhagama na kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo.
Wabunge Aesh Hilaly wa Sumbawanga
Mjini na Mohamed Mchengerwa wa Rufiji wakimsikiliza Waziri Mkuu
Kassim Majliwa wakati alipofungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSFmjini
Arusha Oktoba 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akifungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Jenista Mhagama akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipiga makofi baada ya kupokea tani 45 za saruji zenye thamani ya
shilinigi milioni 15 zilizotolewa na NSSF kabla ya kufungua Mkutano wa
Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimkabidhi, Meneja Mkuu wa Malipo wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), Francis Mcharage cheti cha kuthamini michango ya
wafanyakazi wa shirika hilo kwa NSSF kila mwenzi wakati alipofungua
Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano
cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Watatu kushoto ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na wapili kushoto ni Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiteta na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta
ya Hifadhi ya Jamii, Irene Isaka baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa
Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony
Mavunde na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni
964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko
ya hifadhi ya jamii nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF
ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC),
Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600.
Amesema sekta hiyo imekua kwa
asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia sh. trilioni
10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi ya
wanachama imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko
zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha
mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya
wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja
mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni 9.29,” ameongeza.
Waziri Mkuu pia amemuagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof.
Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika
hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na wale ambao
hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na yeye apewe
taarifa.
“Kumekuwepo na changamoto ya muda
mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta
usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala
hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini
waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza.
Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri
Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote
wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda
uliopangwa wafikishwe mahakamani.
“Nimeambiwa pia lipo tatizo la
wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa
maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na
bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi
wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa
watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”
Akizungumzia utendaji wa shirika
hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya
Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari
nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira zaidi
ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa
NSSF.
“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF
na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa
hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari
kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika
eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,” amesema.
Mapema, akielezea utendaji wa
shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara alisema
limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000 hadi sh. 100,000
kwa mwezi.
Alisema limeanza kufanya upembuzi
yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi Dodoma ili kuendana na uamuzi wa
serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado unaendelea lakini tumeshabaini
kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200 hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.
Kuhusu uwekezaji kwenye ujenzi wa
Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, Prof.
Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa kwa sababu makusanyo ya tozo kwa
watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna uhakika kwamba fedha
tulizowekeza zitarudi,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amepokea msaada wa tani 45 za saruji ambazo ni sawa na mifuko 900 yenye
thamani ya sh. milioni 15 kwa ajili ya waathirika wa tetememo la ardhi
mkoani Kagera. Amepokea msaada huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe.
Akiwasilisha msaada huo, Prof.
Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na wameamua
kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa hayo.
Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya
sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali.
Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 20, 2016.
Tags
HABARI KITAIFA