| Waziri Mkuu Kasmu Majaliwa akitembelea katika viwanja vya hospital ya mkoa wa Dodoma alipofanya ziara ya kwanza baada ya kiongozi huyo kuhamia mjini humo siku moja iliyopita |
| Majaliwa akimjulia hali mama wa mtoto aliyekuwa kalazwa katika wodi ya watoto hospitalini hapo PICHA ZOTE NA JOHN BANDA WA BANDA BLOG |
| Waziri mkuu akitoa maelekezo ya usafi katika maeneo ya hospitali ya mkoa wa Dodoma |
| Baadae akapata nafasi ya kuzungumza na wafanyabiashara wa soko la majengo |
| Akizungumza jambo na mfanyabiashara wa nyanya baada ya kutembelea soko la majengo |
| Muuza Bucha akipokea Fedha toka kwa Waziri mkuu majaliwa baada ya kumuungisha kilo 4 za kitoweo cha nyama wakati alipotembelea soko la majengo |
| Mkurugenzi wa CDA Paskas Mulagili akimuelekeza jambo Waziri mkuu Majaliwa wakati alipokuwa akimuonyesha Ramani ya Magorofa yanayofanyiwa Ukarabati Mkubwa ya Kikuyu mjini Dodoma |
| akiongea na muuza Dagaa wa soko la majengo |
| Akijiandaa kununua Nyama katika moja ya mabucha yaliyopo soko la majengo |
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma lifanye
marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa
kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
Amesema
anatambua maamuzi ya Baraza hilo ni ya kikao halali lakini hakubaliani na
ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea
soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini
Dodoma.
Amesema
soko hilo linatakiwa liboreshwe ili liwe kwenye hali nzuri na Manispaa
ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.
“Kwa
kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na Baraza la
Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika Baraza lenu na
muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.
“Hali
hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa
Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu
na mje mnieleze mmekubaliana nini,” amesisitiza.
Pia
ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo
yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija. Amewaagiza
Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wawachukulie hatua wote watakaobainika kuiba
fedha hizo.
Amesema
Manispaa hiyo inatakiwa kujenga masoko mapya makubwa katika maeneo ya Nkuhungu,
Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili kupunguza msongamano wa
wafanyabiashara katika soko hilo kuu na kusambaza huduma maeneo ya nje ya mji.
Mapema,
akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko
hilo kuwa ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na
shughuli za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi
150,000 kwa mwezi,” alisema huku akishangiliwa.
Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya
maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa nje ya soko na kwenye maeneo
yasiyo rasmi na kusababisha wateja wasiingie sokoni.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametembelea Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi za
wagonjwa, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).
Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na
kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unamwezesha
mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika, mwenza wake na
watoto/wategemezi wanne na Serikali inajazia kiasi kile kile alichochangia.
Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa
wa Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na
miundombinu iliyopo hivi sasa.
Aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika
utendaji kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.
“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa
kazi mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na
kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,” alionya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, OKTOBA MOSI, 2016
Tags
HABARI KITAIFA
