BANDA MEDIA BLOG

SIMBA CHAWENE AZITAKA MAMLAKA ZA SERIKALI KUWACHUKULIA WAMACHINGA KAMA FURUSA NA SI CHANGAMOTO

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene  akitoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu agizo alilolitoa Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli  hivi karibuni juu ya kusitisha zoezi la kuwahamisha Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu Wamachinga na maelekezo kuhusu kurudishwa kwa shule za bweni za Makuyuni (Arusha) na Milundukwa (Rukwa) kwa wamiliki wake ambao ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kulia kwake ni Mkurugenzi Idara ya Tawala za Mikoa TAMISEMI Bi.Susan Chekani na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dkt. Zainab Chaula

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.George B. Simbachawene akitoa Agizo juu ya Shule za Sekondari za Makuyuni (Arusha) na Milundikwa (Rukwa) ambazo majengo yake yalikuwa ni makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadae Halmashauri zikapewa kuyatumia majengo hayo kama shule za Bweni na kwa sasa zinarejeshwa tena mikononi mwa Jeshi kutokana na kuongezeka kwa  shughuli za Jeshi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.George B. Simbachawene akitoa maelezo kwa waandishi wa habari juu ya kutoeleweka vema Agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuhusu zoezi la usitishaji wa kuwaondoa Wafanyabiashara ndogo ndogo katikati ya miji na kuwatafutia maeneo rafiki kufanyia biashara zao kushoto kwake ni Naibu Katibu TAMISEMI (Afya) Dr. Zainab Chaula.




Waziri wa Nchi  Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George B. Simbachawene (Mb) ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini wajipange kutekeleza usimamizi wa agizo ya Mheshimiwa Rais la kuwaondoa  Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu Wamachinga  kwa ufasaha,  weledi na umakini mkubwa ili kusaidia kufanya biashara zao za kujipatia kipato na Mamlaka zote ziwachukulie wamachinga kama fursa na siyo changamoto.
 Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo  mjini Dodoma leo wakati akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake juu ya ukiukwaji wa agizo la Mhe. Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la tarehe 6 Desemba, 2016 kuhusu  zoezi la kusitisha uhamishaji wa Wafanyabiashara ndogondogo maarufu wamachinga.
Mhe. Simbachawene aliongeza kuwa maagizo ya Mheshimiwa Rais yanaonesha ambavyo anawependa na kuwathamini wamachinga hivyo,  wasiondolewe kwenye maeneo  yao kwa sasa hadi watakapotengewa maeneo mbadala, utaratibu wa kuwapangia maeneo uzingatie ushirikishwaji, pale inapowezekana wanaweza kupangiwa  maeneo katikati ya mji  na pia wawekewe utaratibu wa kupangiwa maeneo ya shughuli zao yenye miundombinu rafiki, wateja wa kutosha na pia  washirikishwe  wakati wa maandalizi ya maeneo hayo.
Aidha Mhe. Simbachawene amewataka Wafanyabiashara hao kutafsiri agizo la Mheshimiwa Rais kama fursa kwao na kwamba Mhe. Rais anawathamini na kuheshimu mchango wao katika  uchumi wa Taifa lakini pia  Mhe. Rais hakumaanisha kuwa wafanye biashara  zao mahali popote kiholela  bila kuzingatia sheria zilizopo bali watambue haki za watu wengine  katika kufanya shughuli zao.
Kwa upande mwingine Mhe. Simbachawene amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Rukwa na Arusha ambako kuna shule za bweni za Makuyuni (Arusha) na Milundikwa (Rukwa) wanawatafutia shule wanafunzi waliopo katika shule hizo kwa sasa ndani ya mikoa walipotoka wakishirikianna na Makatibu Tawala wa mikoa husika ili wapangiwe shule mapema na wajue shule watakazo pelekwa kabla ya muhula mpya mwezi, januari, 2017   pia zoezi hili kutowavuruga wanafunzi wa kidato cha sita ambao tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kufanya mtihani wa Taifa mwaka ujao.
Aidha, amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa hiyo kuhakikisha kuwa walimu na watumishi wasio walimu ambao walikuwa wanafundisha katika shule hizo wanapangiwa shule zitakazopokea wanafunzi hao ili kutoathiri mwendelezo wa mada walizokuwa wakifundisha.
Awali majengo ya shule hizo yalikuwa   makambi ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) na baadae Halmashauri zilipatiwa kuyatumia majengo hayo kama shule za sekondari za bweni lakini kutokana na kuongezeka kwa shughuli za Jeshi, Serikali imelazimika kuwahamishia wanafunzi katika shule nyingine zilizopo katika mikoa  waliyotoka.


Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG