
Na.Alex Mathias,Dar es salaam.
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara wameanza vema mzunguko wa pili baada ya kuwatandika wanajeshi JKT Ruvu Stars jumla ya magoli 3-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku zikisomana kwani zilikuwa na mabenchi mapya wenyeji Jkt Ruvu wapo chini ya kocha Bakari Shime na Yanga wapo chini ya George Lwandamina ambaye amechukua mikoba ya Hans Van Der Pluijm aliyepandishwa na kuwa Mkurugenzi
wa ufundi.
Yanga walipata goli la kwanza baada ya beki wa Ruvu Michael Aidan kujifunga dakika ya 38 baada ya pasi ya Simon Msuva aliyepiga shuti kali liloenda moja kwa moja na katika harakati za kuokoa ndipo mchezaji huyu alijifunga hadi mapumziko vijana wa Lwandamina walikuwa mbele.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko hata hivyo hayakuweza kuwasaidia wenyeji mnamo dakika ya 57 Simon Msuva alifunga goli la pili akipokea pasi ya Haruna Niyonzima ambaye alikuwa na kiwango cha juu kabisa kwenye mchezo huo.
Katika dakika za mwisho Yanga waliweza kuutawala mchezo na kucheza pasi za kuonana kutoka kuingia kwa kiungo mkabaji Juma Makapu aliyechukua nafasi ya Amis Tambwe na dakika ya 90 Simon Msuva alipigilia msumari wa tatu baada ya kufunga goli maridadi akipokea tena nafasi ya Niyonzima hadi mwamuzi anamaliza mpira Yanga wameibuka na ushindi wa magoli 3-0.
Kwa matokeo hayo Yanga wamepanda kileleni mwa Ligi wakiwa na pointi 36 na kumuacha Simba mwenye pointi 35 ambaye kesho atacheza na Ndanda Fc kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara huku Simon Msuva naye akilingana na Shiva Kichuya wote wakiwa na magoli 9 kila moja.
Matokeo mengine ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara ni kama unavyoona-Mwadui FC 1-0 Toto African,Ruvu Shooting 1-1 Mtibwa Sugar,Mbeya City 0-0 Kagera Sugar.
Tags
MICHEZO KITAIFA