WAKATI CUF leo ikiadhimisha miaka 16 ya kumbukizi ya mauaji na
ukiukwaji wa haki za binadamu, imeihadharisha CCM na Rais John Magufuli
kutofanyia mzaha matumizi makubwa ya nguvu za Dola kuendesha shughuli za
kidemokrasia na uchaguzi nchini.
Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa
Haki za Binadamu na Sheria wa CUF, Pavu Abdallah Juma, ilisema
wanalaani mauaji ya raia wasio na hatia na vitendo vyote vya ukiukwaji
wa haki za binadamu vilivyofanywa na Serikali ya CCM.
“Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa misingi ya haki,
sheria na uadilifu, badala yake linatumika kama mkono wa kulazimisha
ushindi wa CCM katika uchaguzi na kufanya kazi zake kisiasa zaidi,
badala ya kutanguliza uzalendo na weledi,” alisema Juma kwenye taarifa
hiyo.
Aidha, iliitaka Serikali kutambua kuwa wananchi wamechoka uonevu na
ukiukwaji wa haki za binadamu na wamechoka kunyanyaswa na kushindwa
kuheshimiwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, misingi ya
demokrasia na uchaguzi huru na wa haki.
Iliionya Serikali ya CCM na vyombo vya Dola kutoirejesha nchi kwenye
matukio ya Januari 26 na 27, 2001 ambayo yalisababisha umwagaji wa damu
na mauaji ya raia wasio na hatia.
Alisema CUF itaendeleza juhudi za kuhakikisha migogoro ya kisiasa
inapata ufumbuzi kwa njia ya kidemokrasia na amani, na kuunganisha
Wazanzibari na Watanzania kwa kuwa kitu kimoja na kutanguliza maslahi
mapana ya nchi.
Aidha, ilitoa shukrani kwa viongozi, wanachama, wapenzi na wananchi
wakazi wa Zanzibar kwa uvumilivu ambao unadhihirisha ukomavu wa hali ya
juu wa kisiasa, licha ya hujuma, mauaji, uchokozi na usumbufu wa
makusudi uliofanywa na Jeshi la Polisi na vyombo vya Dola na vikosi vya
ulinzi.
Taarifa ilieleza kuwa CUF itaendelea kushirikiana na vyama vingine vya
siasa, wadau wanaounga mkono kuheshimiwa kwa demokrasia na misingi ya
utawala bora ili kuhakikisha Serikali ya CCM inaheshimu demokrasia na
Watanzania wanapata tume huru za uchaguzi na Katiba inayotokana na
ridhaa yao.
Ilibainisha, kwamba madai hayo yanaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa
ambayo ilishiriki kwenye uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka
juzi, ambapo katika ripoti ya waangalizi wa Jumuiya ya Ulaya
walipendekeza hadi 2020 matatizo yaliyopon yawe yamefanyiwa kazi.
Mwaka 2001 wanachama na wafuasi CUF walijitokeza kwenye maandamano ya
kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na kudai Katiba mpya na
tume huru za uchaguzi.
Tags
SIASA
