Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaagiza
wakurugenzi, waratibu wa Tasaf, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na
wenyeviti wa vijiji Mkoani humo kuhakikisha kwamba haki inapatikana katika
kufanya mchujo kwa zile kaya ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa
kuzinusuru kaya masikini (TASAF)

Ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara yake ya siku ya nne
katika wilaya za kalambo na Nkasi Mkoani humo kwa kuzitembelea kaya za
walionufaika na mpango wa TASAF ambao bado wanaendelea kunufaika na wale ambao
waliondolewa katika mpango huo baada ya kukosa vigezo na hatimae kutakiwa
kurudisha pesa hizo.
“nimezunguka nimebaini kuwa zoezi hili limekuwa likifanyika
hovyo hovyo, hakuna umakini, hakuna usimamizi, hakuna ufuatiliaji, matokeo yake
kwenye mradi wameingizwa watu wenye sifa na wasio na sifa, Wakurugenzi na
waratibu wasimamie zoezi hili, wasiwaachie wenyeviti na watendaji wa vijiji
peke yao katika hili,”
Zelote Stephen alifanya ziara hiyo ili kujiridhisha kuwa kaya
ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa TASAF wanatendewa haki katika kuondolewa
kwenye mpango huo lakini pia kujua sababu zilizopelekea kaya hizo kuingizwa
kwenye mpango bila ya kuwa na vigezo na kuachwa kaya zenye vigezo.
“Wale wote ambao hawana vigezo na kweli ionekane kwamba
hawana vigezo vya kuwepo basi watolewe kwasababau sehemu zingine utakuta kwenye
mpango huo wameingizwa wastaafu, mke wa mwalimu, mjumbe wa smc yumo humo humo,
hii haifai,” Zelote alifafanua.
Katika ziara yake hiyo iliyolenga kufuatilia mchujo wa kaya
hizo, Zelote Stephen alibaini kuwa wakurugenzi pamoja na waratibu wa TASAF
wilaya wanakosa umakini katika kuzifanya shughuli zao na hatimae kubaki maofisini
kusubiri ripoti zitokazo vijijini bila ya kufuatilia kwa kina kwa kufika katika
maeneo husika ili kujua hali halisi.
“Mimi nina taarifa kwamba fedha za ufuatiliaji wa TASAF
zikifika tu katika Ofisi ya Mkurugenzi, kama zimefika asubuhi basi mchana tu
hakuna senti tano, zote zimeshanyanganyiwa na hatimae makusudio ya fedha zile
hayatimii na ufuatiliaji haufanywi,” Alisisitiza.
Nae mratibu wa TASAF Mkoa wa Rukwa, James Kapenulo aliongeza
kuwa kaya zote ambazo zilinufaika na TASAF kwa kuwa na mashamba na nyumba nzuri
ambazo kabla ya TASAF hawakuwa nazo, familia hizo ndio ziwe za mfano na
ziendelee kuwezeshwa ili tathmini itakapokuja kufanywa ioneshe hali halisi ya
mafanikio ya mpango huo.
“Hatuwezi tukaendelea kuwaweka wale ambao wakipewa pesa za
TASAF wanaishia kwenye vilabu vya pombe na kumuacha yule ambae akipewa pesa
hizi ananunua kuku au mbuzi au bati na kuwapeleka watoto shuleni, hayo sio
madhumuni ya mpango huu, huyu aliyefanikiwa baada ya TASAF ndiye ametoka weye
umaskini.
Naye mnufaika wa TASAF aliyetolewa kwenye mpango huo Mathias
Mwanakatwe alimshukuru Mkuu wa wa Mkoa kwa kuweza kuliona hilo na
kulishughulikia kabla hali haijawa mbaya zaidi kwa wale wananchi wenye wivu na
chuki kwa wale waliofanikiwa kutokana na kuwepo kwa mpango huo wa TASAF.
Tags
HABARI KITAIFA

