Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewasili mkoani Dodoma leo asubuhi kwa
ajili kuhudhuria vikao vya bunge ambavyo vinatarajiwa kuanza kesho
Jumanne
Waziri Mkuu ameongozana na mkewe Mary Majaliwa pamoja na viongozi
mbalimbali ambao wametumia usafri wa ndege ya abiria ya ATCL inayopitia
Dodoma kuelekea Kigoma
Katika Uwanja wa Ndege Waziri Mkuu amepokelewa na mkuu wa mkoa wa Dodoma
Jordan Rugimbana pamoja na viongozi wa serikali na chama wa mkoa wa
Dodoma.
Mara baada ya mapokezi hayo, Waziri Mkuu amefungua Kikao cha Baraza la
Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma ambapo amesema kikao hicho ni chombo
muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia kusukuma maendeleo
ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.
Amesema wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha
kwenye Halmashauri zote nchini na pia hazitakiwi kuwa pango la wezi,
wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu walioshindikana kwingineko.
Aidha, Waziri Mkuu amesemma Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini
zinatakiwa zianze kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa
namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vinavyotarajiwa.
Hata hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa
Ilani ya CCM kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa
miundombinu ya shule, maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa
hospitali, zahanati na vituo vya afya).
“Endeleeni kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo
atimize wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni
migogoro, matusi, dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo
wamoja,” amesema.
Vikao vya Bunge vinaanza kesho baada ya wiki mbili za shughuli za kamati
za kudumu za Bunge, na sasa tayari wabunge wamekwishawasili Dodoma kwa
ajili ya vikao hivyo vitakavyodumu kwa takriban wiki 2
Tags
HABARI KITAIFA
