Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema licha ya uchumi wa
Tanzania kukua kwa asilimia saba kwa zaidi ya muongo mmoja, bado hali ya
uchumi ni mbaya Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa takwimu jijini
Dar es Salaam jana, Dk Mpango alisema ili kupambana na umaskini,
Serikali imejikita kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira.
Alitaja takwimu za Benki ya Dunia (WB) za mwaka 2013 akisema asilimia
10.7 ya watu wote duniani ambao ni bilioni 7.1 walikuwa wakiishi chini
ya Dola 1.90 za Marekani kwa siku ikilinganishwa na asilimia 12.4 mwaka
2012. “Mbali na takwimu hizo kuonyesha umaskini kushuka kwa kasi ndogo,
mafanikio hayo hayaonekani waziwazi kwa baadhi ya nchi zinazoendelea
ikiwamo Tanzania,” alisema.
Alisema hali hiyo inatokana na ukuaji wa uchumi kutokana na sekta
zinazoajiri watu wachache na nyingi zikijikita mijini na kuwapo kwa kasi
ya ongezeko la watu.
Tags
Bunge
