Wabunge wa upinzani jana walisusia kikao cha Bunge mjini hapa, wakipinga
kile walichodai ni mhimili huo wa dola kudhalilishwa na kushushiwa
hadhi yake na Jeshi la Polisi.
Tafrani hiyo iliibuka saa 10:22 jioni baada ya Naibu Spika, Dk Tulia
Ackson kukataa hoja ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT -Wazalendo), Zitto
Kabwe aliyetaka Bunge lijadili na kuweka azimio la kadhia hiyo.
Wakizungumza katika viwanja vya Bunge baada ya kutoka ukumbini, wabunge
hao walisema vita hiyo wataiendeleza leo asubuhi, hadi kiti cha Spika
kitakapotoa msimamo wa kulinda hadhi ya mhimili huo.
Kilichowasukuma zaidi wabunge hao kutoka ni hatua ya Naibu Spika,
kuwaamuru askari wa Bunge kumtoa Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa
Ryoba aliyekuwa akipinga uamuzi wa kiti.
Baada ya uamuzi wa Naibu Spika kukataa Bunge lisijadili hoja ya Zitto na
kuweka azimio, wabunge wa upinzani walionekana kupinga kwa kupaza sauti
zao akiwamo Ryoba.
“Mheshimiwa Ryoba naomba utoke mwenyewe. Mheshimiwa Ryoba naomba utoke
mwenyewe,” alisikika Naibu Spika akisema huku Ryoba akisema hatoki ndipo
Tulia akaagiza polisi wamtoe.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani kwa umoja wao ndipo wakaamua kutoka
ukumbini na kuwaacha wa CCM wakiendelea na kikao cha Bunge cha jioni.
Kiini cha sakata hilo ni hatua ya polisi kumkamata Mbunge wa Singida
Mashariki, (Chadema) Tundu Lissu, juzi jioni wakati akitoka bungeni na
jana ilidaiwa polisi walikuwa wakimwinda Zitto.
Tags
Bunge
