Jinsi ambavyo baadhi ya bakteria wasivyo na hofu siku hizi kuhusu
antibiotics, ndivyo ambavyo mbu wamebuni njia mpya ya kujikinga na
chandarua kilichowekwa dawa. Hii ni kutokana na utafiti mpya
uliochapishwa na gazeti la ‘infectious Diseases”.
Utafiti huo uliofanywa kwa miaka minne katika nchi ya Papa New Guinea
ili kuangalia ni kwa namna gani ugawaji wa vyandarua vyenye dawa
vimeweza kusaidia kupiga vita ugonjwa hatari wa malaria.
Vyandarua vilivyopigwa dawa vimeonekana kama njia sahihi na yenye
mafanikio kwenye kupunguza vifo zidi ya ugonjwa hatari wa malaria.
Kutokana na takwimu zilizotolewa na American Council on Science and
Health, kesi (case) tofauti tofauti milioni 451 zimeweza kuzuiwa za
malaria katika miaka 15 iliyopita kutokana na utumiaji wa vyandarua
vilivyowekwa dawa.
Utafiti huu umeonyesha kuwa mbu sasa hivi wamebadili utaratibu wa kuuma
(feeding behavior) katika miaka ya hivi karibuni ili kujiepusha na
vyandarua vyenye dawa.
Kabla ya ugawaji wa vyandarua vilivyowekwa dawa mbu walikuwa na tabia ya
kung’ata kuanzia usiku wa manane. Lakini baada ya watu kuanza kutumia
vyandarua vyenye dawa, mbu wamebadili ratiba yao ya kupata chakula na
kuanza kung’ata kuanzia saa nne usiku (10 p.m) na wengine hung’ata
kuanzia saa moja(7 p.m) mpaka saa tatu usiku (9 p.m). Ili kuwapata watu
kabla hawajaingia ndani ya chandarua chenye dawa.
Kupungua kwa kesi (case) nyingi za malaria kutokana na kung’atwa na mbu
kumefuatiwa na kuongezea tena kwa kesi hizo kiama ilivyokuwa awali kabla
ya mgao wa vyandarua vilivyowekwa dawa kwa baadhi ya maeneo. Utafiti
huo umekuwa unaleta matokeo tofauti tofauti pia katika vijiji tofauti
tofauti.
Nitoe wito kwa watanzania tuendelee kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa
kwani vimeonyesha kupunguza idadi kubwa ya kesi (case) za malaria,
lakini pia tujitahidi kuweka mazingira safi yanayotuzunguka ili kufanya
mazingira yetu yasiwe mazingira salama kwa mbu kuzaliana na kuishi.
Malaria haikubariki, tuungane kutokomeza ugonjwa huu hatari wa malaria.
Your Health, My Concern
Tags
AFYA
