RAIS John Magufuli amewanyoshea kidole Polisi, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa ndio chanzo cha serikali kupoteza
kesi nyingi kutokana na kupindisha na kuwasilisha ushahidi hafifu
mahakamani.
Pia ameagiza mamlaka zinazohusika na kusikiliza kesi, mhalifu ambaye
anakamatwa na vidhibiti, kesi yake isikilizwe siku hiyo na hukumu
kutolewa siku hiyo hiyo badala ya ilivyo sasa waendesha mashitaka
wanarefusha kesi hizo kwa kisingizio cha ushahidi kutokamilika.
Alitumia maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Dar es Salaam jana
kuwanyooshea kidogo majaji katika maamuzi yao waliyoyafanya kuhusu
mahakimu 28 waliokuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya rushwa kuachiwa huru
wote.
Aliziagiza pia ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka kuhakikisha kwamba zinaacha kugombana, kwani
nazo zimekuwa zinachangia kutengeneza ushahidi hafifu na hivyo kufanya
serikali kupoteza kesi mahakamani.
Awapasha Polisi, Takukuru
Alisema Polisi na Takukuru ambao ndio wenye jukumu la kufanya upelelezi
wamekuwa hawafanyi upelelezi na wamefikia hatua wanamkamata mtuhumiwa na
vidhibiti, lakini mtuhumiwa anashinda kesi.
Alitoa mfano kuwa mtuhumiwa wa dawa za kulevya anakamatwa na dawa za
kulevya, lakini akifikishwa mahakamani upande wa mashitaka unashindwa
kuendelea na kesi kwa kisingizio kuwa upelelezi haujakamilika.
“Mtuhumiwa anakamatwa na jino la tembo, lakini wanadai upelelezi bado
kukamilika, au kakamatwa na dawa za kulevya baada ya muda dawa hizo
zikipelekwa kwa mkemia inabainika kuwa ni unga wa muhogo wa huko
Sumbawanga,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kutokana na ushahidi kutokuwepo, mahakama inalazimika kumwachia
huru mtuhumiwa; hivyo akaonya kuwa umefika wakati vyombo hivyo
vijitathmini na vibadilike.
Aliagiza kuwa mtu akishikwa na vidhibiti, siku hiyo hiyo kesi yake
isikilizwe na imalizike, na kama kuna mtu atajitokeza kumtetea naye
aunganishwe kwenye hiyo kesi wote waende jela. Serikali haijalipwa
trilioni 7.5/-.
Alisema majaji watafute namna ambavyo wanaweza kutumia sheria watuhumiwa
wa namna hiyo wahukumiwe kwenda jela, “sheria huwa inasema kifungo au
faini, sasa nyinyi hawa wenye vidhibiti mnawahukumu vyote pamoja.”
Alibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2016,
serikali haijalipwa kiasi cha Sh trilioni 7.5 licha ya kushinda kesi za
ukwepaji kodi zilizokuwa zinawakabili washitakiwa mbalimbali.
“Haiwezekani mwekezaji anachimba madini yetu, kodi halipi, anashitakiwa
mahakamani anashindwa, halafu pesa haitolewi. Sasa tujiulize, kama
utoaji haki unaakisi ujenzi wa uchumi wa nchi ni kwa kiasi gani kesi
zenye thamani ya Sh trilioni 7.5 zimeathiri uchumi?” Alihoji Rais
Magufuli.
Ugomvi wa AG, DPP
Rais Magufuli alitoboa kwamba ofisi hizo mbili muhimu katika utoaji wa
haki nchini watendaji wake wamekuwa wanagombana, jambo ambalo linafanya
serikali ishindwe kesi kutokana na ushahidi hafifu unaowasilishwa na
watendaji wa ofisi hizo.
Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Mkurugenzi
wa Mashitaka ya Jinai (DPP), Biswalo Mganga wamekuwa wakigombana wenyewe
kwa wenyewe na akawataka watendaji wa ofisi hizo kujitathmini wenyewe,
ni wapi wanakosea na wapi wanakwenda kwa kuendekeza ugomvi huo.
“Waziri unafahamu ugomvi wa ofisi hizi mbili, cha ajabu wote hawa
wanatoka mkoa mmoja na yawezekana wilaya moja, sijui wanagombea nini.
Kama ni madaraka wote ni wateuliwa wa Rais, kama ni kasima tafuteni
suluhisho,” alisema Rais Magufuli.
Alionya kuwa bila kutafuta suluhisho, serikali itaendelea kupoteza kesi kutokana na ushahidi laini unaowasilishwa mahakamani.
Alisema wakati mwingine ushahidi unakuwa laini hadi kumfanya jaji
aahirishe kesi kutoa nafasi kwa mawakili wa serikali kwenda na ushahidi
mzito, lakini hawafanyi hivyo.
“Kwa hali unakuta ushahidi upo, lakini tunashindwa kwa sababu ushahidi
unaopelekwa mahakamani ni mwepesi kutokana na matatizo yaliyopo katika
ofisi hizi mbili,” alisema.
Ahoji mahakimu kutofungwa Katika hotuba yake, Rais Magufuli alihoji
mahakimu 28 walishitakiwa kwa tuhuma za kupokea rushwa, lakini
akashangaa kwamba katika kesi zote hizo hakuna hakimu hata mmoja
aliyetiwa hatiani na kufungwa.
Alisema kwa hali ya kawaida raia ambao sio wanasheria wanakuwa na
maswali mengi kuhusu maamuzi hayo ya mahakama. Alisema yawezekana
upelelezi wa polisi haukufanywa vizuri au ushahidi ulikuwepo, lakini
haukufikishwa vizuri mahakamani.
“Yawezekana mawakili wa pande zote walikula njama kuhakikisha hakuna
ushahidi unaotolewa dhidi ya mahakimu hao au yawezekana majaji au
mahakimu wenzao waliamua kuwaachia huru wenzao kuthibitisha ule usemi
kuwa kesi ya ngedere unampelekea nyani,” alibainisha Rais Magufuli.
Alisema jambo hilo ni changamoto kwa Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu
Juma na alimtaka ashughulikie suala hilo kwani mbele ya wananchi maamuzi
hayo ya mahakama yanaleta shaka na akawataka majaji wajipange kuondoa
changamoto hizo wanapoanza mwaka mpya wa mahakama.
Alisema Watanzania wangefurahi hata mahakimu wawili wangefungwa.
Rais Magufuli pia alisema kuna madudu mengi yanafanywa ndani ya Idara ya
Mahakama, lakini yamekuwa yanapita kimya kimya na akatolea mfano baadhi
ya majaji kuhusishwa kupokea fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow katika
Benki Kuu (BoT), lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya
majaji hao.
Alisema mambo kama hayo yanaumiza kuona yanafanywa na chombo ambacho kina dhamana ya kutoa haki ya kisheria kwa wananchi.
Alisema kuna majaji wachache sio waadilifu ambao wamekuwa wanaichafua
sura ya mahakama “Yawezekana hapa asilimia 99.99 ni wasafi, lakini
wanachafuliwa na hawa wachache ambao ni asilimia 0.00. Jaji Mkuu
tafadhali chukua hatua dhidi ya watendaji hawa wachafu,” alisema
Magufuli na kuongeza kuwa ameyasema hayo kwa sababu mahakama haiongozwi
na malaika.
Alisema kuna majaji kutokana na uchafu wao, tangu waanze kusikiliza
kesi, Serikali haijawahi kushinda kesi zinazofikishwa “Unajiuliza hivi
kesi zote huwa hazina ushahidi? Ashangaa kuhusu ajira mpya.
Akijibu maombi ya Jaji Juma kutaka mahakama iruhusiwe kuajiri watumishi
wapya wapatao 900, Rais Magufuli alishangaa kwani kwa sasa taasisi hiyo
ina watumishi 6,500 ambao ni wengi kuliko idara nyingine serikalini na
akahoji iweje watake kuongeza watumishi.
“Ninyi ndio wengi kuliko idara nyingine yoyote, kwa mfano mnataka
walinzi wa nini, hivi polisi hawalindi mahakama, kama hawalindi kwa nini
msitoe kwa kampuni binafsi za ulinzi?Angalieni nani anahitajika katika
mageuzi haya mnayofanya,” alisema Rais Magufuli.
Pia aliishauri idara hiyo kuhakikisha kwamba inaunganisha baadhi ya
shughuli ambazo zilikuwa zinafanywa na watu wanne ifanywe na mtu mmoja
na aongezewe mshahara badala ya kutaka kuongeza watumishi wengine wapya.
Alisema inamuwia vigumu kuongeza ajira za umma kwa sababu Serikali
inatumia Sh bilioni 600 kila mwezi kuwalipa wafanyakazi 546,166 kila
mwezi na bado kuna kulipa madeni mengine jambo ambalo linafanya serikali
inalemewa.
Alitoa mfano kuwa mwezi uliopita serikali ilifanya malipo ya mishahara
na kulipa madeni yenye thamani ya Sh bilioni 955 wakati makusanyo kwa
mwezi ni Sh trilioni 1.2. Alitahadharisha kuwa suala la kuongeza
watumishi wapya linaweza kufanya Serikali ishindwe kuwalipa mshahara.
Alisema atawaruhusu mahakama kuajiri watumishi wa kada zinazotakiwa tu
na akamtaka jaji mkuu kuhakikisha kwamba kwa nafasi ambazo sio muhimu
wafanye mageuzi waangalie namna ya kuzijaza nafasi hizo kwa kutumia
watumishi waliopo.
Ataka mawakili kuwa wazalendo Rais Magufuli pia aliwaagiza mawakili
kuhakikisha wanakuwa wazalendo na wawatose watuhumiwa wabaya na
wasiwatetee.
Alisema wahalifu hao wabaya wakitaka wawatetee, mawakili wachukue fedha
zao lakini wakifika mahakamani wawaruke “Chukueni fedha zao, lakini
mkifika mahakamani wageukeni,” aliwaambia.
Pia aliwataka mawakili hao kupitia chama chao, Tanganyika Law Society
(TLS) kuacha kujihusisha na siasa badala yake wasiwe na vyama katika
kutekeleza majukumu yao.
Alisema ndani ya TLS kumekuwa kama chama cha siasa, hadi kwenye kampeni
za uchaguzi wanapigana mkumbo watu wenye mlengo tofauti wa vyama vya
siasa. Alisema yeye hatakuwa tayari kuteua wakili kuwa jaji ambaye
anashabikia vyama vya siasa.
“Jijengeeni heshima kwa kuwa neutral (msiwe na upande), hiyo itawajengea heshima,” alisema Rais Magufuli.
Mwanamama azua tafrani, aibukia kwa Rais
Katika hatua nyingine, mwanamke mkazi wa Tanga, Sobha Mohammed alizua
tafrani baada ya kuibuka mara tu Rais alipomaliza hotuba yake akiwa na
bango, lakini kabla ya kufika mbele ya meza kuu alikumbana na rungu la
walinzi wa rais.
Mama huyo alirejeshwa nyuma kuondolewa eneo hilo huku watu waliokuwapo
hapo wakishuhudia, na wakati huo Rais Magufuli alikuwa katika mazungumzo
na Kaimu Jaji Mkuu, lakini baada ya muda mfupi kulitokea agizo la Rais
la kutaka aachwe na apelekwe kwao atoe kilio chake.
Alipofika mbele, mama huyo alianza kutoa kilio, na akielezea madhila ya
kudhulumiwa haki zake katika kesi iliyofunguliwa mkoani Tanga na kwamba
amefika katika ofisi mbalimbali za wahusika wa masuala ya kisheria
kuanzia Polisi hadi kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison
Mwakyembe.
Baada ya kumsikiliza mama huyo, Rais Magufuli aliagiza, “Ofisi ya DPP,
AG na…. Jaji Kiongozi si ndio msimamizi wa kesi zote za chini chini, si
ndio bwana. Shughulikie suala la huyu mama. Kama kesi iko Mahakama ya
Mwanzo kule muivute huku haraka haraka, ishughulikiwe haraka.
Na AG pia mshughulikie, lakini na pia mumlinde ili asidhuriwe kwa kifo
cha aina yoyote. Chukua jina lake, lakini pia mtafutieni Polisi ili
amlinde. Lakini mhakikishe usalama wake. Jaji Kiongozi chukua simu yake.
Na mama njoo uchukue simu ya Jaji Kiongozi, umpigie moja kwa moja.”
Kauli ya Rais ilipokewa kwa shangwe na nderemo. Profesa Lipumba apongeza
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema
kitendo cha Rais kuyasema mambo hayo hadharani hapo, kinaonesha kuwa
anataka kupata nguvu ya kisiasa ili wananchi wajue kinachoendelea katika
mfumo wa utoaji wa haki nchini.
“Kwa mfano, serikali imeshinda kesi na inatakiwa kulipwa shilingi
trilioni 7.5, lakini hazijalipwa tatizo liko wapi? Alihoji Lipumba.
Profesa Lipumba alisema kuna haja ya watendaji ndani ya mfumo wa
mahakama na vyombo vingine vya serikali kuhakikisha kwamba wanabadilika
ili mapungufu aliyoyaainisha Tais yasiwepo tena.
Tags
HABARI KITAIFA
