MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) ametishia kuwa endapo
wananchi wake hawatopata maji kutoka chanzo cha maji cha Ihelele kama
walivyoahidiwa na serikali, ataongozana na wananchi hao kwenda kuzima
mitambo ya maji katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, chanzo hicho cha maji kwa sasa kinazalisha
maji yanayopelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shinyanga na Kahama
kupitia Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Kahama na Shinyanga
(Kashuwasa).
Akiuliza swali la nyongeza bungeni Dodoma mbunge huyo alisema tangu
serikali iwaahidi kuwa jimbo hilo la Misungwi litapata maji kupitia
mradi huo wa maji wa Ihelele hadi sasa maji hayo hayatoki wakati maeneo
mengine yanapata.
“Naibu Spika nasema wazi kuwa nitaongozana na wananchi wa jimbo langu
kwenda kuuzima ule mtambo wa maji Ihelele kama maji haya yataendelea
kutotoka kwenye maeneo yetu,” alisema Kitwanga ambaye aliposimama
kuuliza swali hilo alishangiliwa sana na wabunge wenzake.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge
alimtaka mbunge huyo asiandamane na wananchi wake, kwani kilichokwamisha
maji hayo yasifike jimboni kwake ni uhaba wa fedha za kuunganisha bomba
la maji hadi eneo hilo ambapo zinahitajika takribani Sh bilioni nne.
Tags
HABARI KITAIFA
