WIZARA Maliasili na Utalii inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya
kufukua nyayo za Laetoli zilizopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
zilizogunduliwa na mtafiti Dk Mary Leakey mwaka 1978.
Jitihada hizo za wizara zinafanywa kutokana na agizo la Rais wa Awamu ya
Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2007, alipoitaka wizara hiyo kufukua nyayo
hizo na kuzihifadhi kisasa kwa matumizi ya elimu na utalii kwa
Watanzania na wageni.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alikuwa akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mchafu Chakoma (CCM) aliyetaka kujua
serikali inafanya mkakati gani kuajiri wataalamu wa kufukua nyayo hizo.
Makani alisema, mradi huo una gharama kubwa unakadiriwa kugharimu dola
za Marekani milioni 50 (sawa na Sh bilioni 105), ambazo zitatumika kwa
ajili ya kusomesha wataalamu na kuandaa michoro ya ujenzi wa makumbusho.
Lakini pia fedha hizo zitatumika katika kufufua na kuhifadhi nyayo hizo,
kusimamia ujenzi na kuweka mifumo ya uhifadhi wa kisasa wa nyayo hizo.
Alisema fedha hizo ni nyingi, ukilinganisha na mapato na majukumu ya
mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambayo inatakiwa kugharamia, hivyo
wizara inaendelea kutafuta fedha ili kugharamia utekelezaji wa mradi
huo.
Makani alisema hakuna hali ya kusuasua katika kutekeleza mradi huo kwani
baadhi ya kazi tayari zimekwisha kamilika na nyingine zipo katika hatua
mbalimbali za utekelezaji. Kazi zilizokamilika ni pamoja na kuundwa kwa
idara ya urithi wa utamaduni, kukamilika kwa michoro ya awali ya jengo
la mapokezi, jengo la utafiti na jengo la elimu kwa umma.
Pia imewasilishwa tathmini ya athari kwa mazingira kwa mamlaka husika
ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa uchambuzi wa kina ili kutoa idhini na
kutoa mafunzo ya shahada ya uzamivu kwa watumishi wawili.
Kazi ambazo zinaendelea kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za
ajira kwa baadhi ya watalaamu wanaopatikana nchini na kukusanya takwimu
sahihi kuhusu mazingira rafiki ya nyayo hizo na kazi inafanywa na
watalaamu kutoka nje ya nchi inatarajiwa kukamilika Februari mwaka huu.
Tags
UTALII
