
Wakati wafanyakazi jana walisherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei
Mosi’, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ziito Kabwe, ameleeza
kilio chake kuhusu makato ya mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na
jinsi kampuni zinavyopoteza asilia 5 la pato la taifa.
*** Hizi ni Salaam za Kiongozi wa ACT Wazalendo Kwa Wafanyakazi wa Tanzania, Mei Mosi 2017
Ndugu Wafanyakazi
Leo (JANA )ni siku yenu katika mwaka. Kama ilivyo kawaida siku hii
husherehekewa kwa maadhimisho makubwa ambapo Waajiri (Serikali na Sekta
Binafsi) na waajiriwa hutoa hotuba mbalimbali. Wakati mwengine ni siku
kama siku nyengine tu za miaka ya nyuma, hotuba, ahadi, kula na kunywa.
Hata hivyo Wafanyakazi wa Tanzania wana changamoto nyingi sana na ni
vema kutumia siku hii kutafakari Kwa kina changamoto hizi na kutafuta
majawabu yake.
Sisi ACT Wazalendo tunaamini katika siasa za Kijamaa, siasa zenye
kupigania zaidi maslahi ya wanyonge, Wafanyakazi, Wakulima, Wavuvi na
Wakwezi. Katika salaam zangu mwaka huu nawaomba mtafakari hotuba yangu
hii niliyotoa Arusha tarehe Machi 25, 2017 na mapendekezo machache
ninayoyatoa mwishoni mwa waraka wangu huu kwenu.
Nchini Tanzania Wafanyakazi kwenye sekta rasmi ni milioni 2.1 sawa na 9%
tu ya nguvu kazi yote ya Taifa. Hawa wameajiriwa kwenye sekta binafsi
(1.4m sawa na 67%) na sekta ya umma (700,000 sawa na 33%). Hawa
wanalipwa mishahara na posho mbalimbali kama chanzo cha mapato yao.
91% ya Watanzania wapo kwenye sekta isiyo rasmi na rekodi ya mapato yao
yaweza kuwa kizungumkuti kuipata. Hata hivyo tunajua kuwa wengi
wameajiajiri wenyewe kwenye kilimo na biashara ndogo ndogo, uvuvi,
ufugaji, uchimbaji wa madini na utoaji huduma.
Ni muhimu kusisitiza kuwa Watanzania wengi hawamo kwenye ajira rasmi au
isiyo rasmi. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 inaonyesha
kuwa Jijini Dar es Salaam kwa mfano ni asilimia 60 tu ya wakazi wake
wapo kwenye ama ajira rasmi au ajira isiyo rasmi na asilimia 40 hawana
kazi yeyote.
Uchambuzi pekee ambao tunaweza kuufanya kwa sasa ni kwa kutumia vyanzo
vya mapato ya serikali ambapo tutaona mchango wa Wafanyakazi kwenye
mapato ya Serikali kulingana na vyanzo yake vya mapato.
Kwa mfano, Kitabu cha Mapato ya Serikali Kuu cha mwaka 2016/17
kinaonyesha kuwa Wafanyakazi wote wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi
watachangia jumla ya shilingi trilioni 3 kwenye mapato yote ya Serikali
kulinganisha na wenye mitaji (waajiri) ambao watachangia jumla ya
shilingi bilioni 900 tu kutoka kwenye kodi za faida/gawio, ongezeko la
mitaji na riba (taxes on income/interests, profits and capital gains).
Hata ukitazama miaka miwili ya nyuma utaona kwamba mwaka 2015/16
makampuni yalichangia shilingi 773 bilioni wakati Wafanyakazi
walichangia shilingi 2.2 trilioni na mwaka 2014/15 makampuni yalichangia
shilingi 600 bilioni na wafanyakazi shilingi 1.9 trilioni kama kodi zao
kwenye mapato ya Serikali. Kwa kutumia kigezo cha Kodi za Mapato,
matajiri (waajiri) wanachangia robo tu ya mapato yote ya serikali na
wafanyakazi wanachangia robo tatu iliyobakia. Hii inachangia sana kuwepo
kwa tofauti ya kipato ndani ya jamii.
Kwanini wafanyakazi wanachangia zaidi kuliko wenye mitaji ni swali
ambalo tutalieleza. Sababu kubwa ni kuwa wenye Miraji/Mabepari wana
fursa ya kukwepa kodi kisheria wakati wafanyakazi hawana uwezo huo. Kodi
za wafanyakazi hukatwa moja kwa moja na waajiri kutoka kwenye mishahara
yao.
Kwanini Kodi za Makampuni ni kidogo kuliko za Wafanyakazi?
Wafanyakazi wao hukatwa kodi zao kutoka kwenye mishahara yao moja kwa
moja ikiwemo pia makato mengine kama michango kwenye mifuko ya Hifadhi
ya Jamii na Bima ya Afya. Makato hayo huanzia asilimia 9 kwa mishahara
ya ngazi ya chini mpaka asilimia 30 kwa wenye kulipwa mishahara ya juu
kabisa. Kwa hiyo kodi ya wafanyakazi ni kodi ambayo serikali ina uhakika
nayo moja kwa moja. Kwa takwimu ambazo tumeziona tayari, ni wafanyakazi
wa sekta rasmi tu ndio hubeba mzigo wote wa kodi za wafanyakazi hapa
nchini. Lakini kwanini kodi zinazotokana na mapato ya makampuni ziwe
kidogo kuliko kodi zinazotokana na mapato ya wafanyakazi?
Kwenye makampuni, Kodi ya Mapato ni asilimia 30 ya faida ambayo kampuni
imepata. Lakini mapato yanayokusanywa kwenye kodi hii ni kidogo sana
kama tulivyoona, shilingi bilioni 900 tu kati ya mapato yote ya serikali
mwaka 2016/17 sawa na asilimia nne tu ya mapato yote ya serikali
yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali halisi hii sio ya
Tanzania peke yake.
Mwanazuoni Thomas Piketty anaeleza kuwa "Ingawa kodi za faida za
makampuni ni kati ya asilimia 40 - 50 kwenye nchi za magharibi, mapato
kwenye kodi hizi hayazidi asilimia 2.5 - 3 ya Pato la Taifa. Nadharia ya
faida inayotozwa kodi ni nyembamba kuliko nadharia ya mapato ghafi ya
ziada kwa sababu makampuni huondoa gharama za uchakavu wa mitambo, riba
kwa mikopo na hata gharama za bima. Kodi kwenye faida imegubikwa na
matundu mengi kwenye mfumo mzima wa kodi duniani" (msisitizo ni wangu).
Matundu haya ndiyo njia za ukwepaji kodi zinazofanywa na makampuni na
hasa makampuni ya kimataifa (Multinational Corporations). Nchi za Afrika
zimeathirika mno na mfumo wa kodi wa kimataifa na hivyo kupelekea fedha
nyingi kutoka Afrika kutoroshwa kwenda ughaibuni. Azimio la Tabora la
Chama cha ACT Wazalendo limeeleza kidogo kadhia hii ambayo Serikali za
Afrika hazitilii maanani kabisa licha ya taarifa nzuri ya Rais mstaafu
Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini.
Katika kitabu cha 'Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans &
Capital Flight Bled a Continet' waandishi Leonce Ndikumana na James
Boyce, wameonesha kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, jumla ya
dola za Kimarekani bilioni 11.4 (wastani wa shilingi trilioni 24)
zimetoroshwa kutoka Tanzania kwa njia mbalimbali.
Hizi ni sawa na wastani wa dola za Kimarekani 285 milioni kutoroshwa
kila mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi
zinatoroshwa na makampuni makubwa ya kigeni yanayofanya biashara na
kuwekeza hapa nchin. Africa Progress Panel na kikosi kazi kilichoongozwa
na Rais Thabo Mbeki ilieleza kuwa Afrika hupoteza zaidi ya dola za
kimarekani bilioni 50 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha
unaofanywa hususan na makampuni haya ya kimataifa.
Inasemekana asilimia 30 ya utajiri wa fedha wa bara la Afrika umewekwa
kwenye pepo za kodi (tax havens) kwa mujibu wa kitabu cha 'The Hidden
Wealth of Nations' kilichoandikwa na Gabriel Zucman, mhadhiri wa London
School of Economics.
Katika kitabu hicho, Zucman ameonyesha takwimu kutoka Benki ya Taifa ya
Uswisi zinazothibitisha kuwa takribani dola za kimarekani bilioni 150
kutoka Afrika zimehifadhiwa kwenye mabenki ya nchi hiyo. Jumla ya Pato
la Taifa (GDP) ya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni dola za
kimarekani 147.3 bilioni, hivyo fedha za Afrika zilizopo Uswisi ni zaidi
ya GDP ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja. Fedha
hii ni mara tano ya gharama za kujenga mradi wa Inga Dam kule Kongo
ambao ungeweza kuzalisha umeme wa kutosha bara zima la Afrika.
Pamoja na mambo mengine, matundu haya ya ukwepaji kodi yamejengwa ndani
ya mfumo wa kodi za kimataifa. Kuna kitu kinaitwa kwa lugha ya kigeni
Base Erosion and Profit Shifting ikiwa na maana kuwa makampuni ya
kimataifa yanapowekeza hapa nchini huhamisha faida kupeleka nchi zenye
viwango vidogo vya kodi na hivyo kutolipa kabisa kodi hapa nchini ama
kulipa kodi kiduchu sana.
Kwa mfano, katika kukokotoa kodi kampuni huondoa gharama za riba za
mikopo, bima na gharama za utawala na kinachobakia ndio faida ambayo
hutozwa kodi. Kampuni hizi huchukua huduma hizi za mikopo, bima na
utawala kutoka kwa makampuni dada na kuongeza gharama maradufu na hivyo
kuhamisha fedha hizi kana kwamba wanalipia hizi gharama na hivyo
kupunguza sana wigo wao wa kodi. Ndio maana siku za nyuma tulisikia
kampuni za madini hazilipi kodi ya mapato kwa sababu nyingi zilikuwa
zikitumia mtindo huu wa kumomonyoa wigo wa kodi.
Wakati nikiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Madini ya Jaji Mark Bomani
tulikuta ushahidi wa kampuni ya Geita Gold Mines ambayo uwiano wa mtaji
wake na mikopo (debt-equity ratio) ulikuwa asilimia milioni 12. Hii
iliifanya kampuni hii kumomonyoa kila walichokipata katika uchimbaji wa
dhahabu nchini kwetu na kukihamishia njia kana kwamba ni malipo ya
mikopo waliyochukua kumbe ni mbinu ya kukwepa kodi na kupora dhahabu ya
Tanzania. Nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali, tuliagiza ukaguzi wa ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya
kimataifa na iligundulika kuwa karibia kila sekta ya uchumi ilihusika na
ukwepaji kodi.
Mfano ambao huwa naukumbuka mara kwa mara ni mfano wa mauzo yetu ya
Korosho kwenda nje. Hupenda kuurudia na nitaurudia tena hapa. Mwaka 2011
Tanzania iliuza Korosho kwa nchi ya India. Kwenye rekodi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania ilionyesha kuwa tuliuza tani 80,000 za korosho kwa bei
ya dola za marekani 1000 kwa kila tani sawa na dola za kimarekani 80
milioni.
Uchunguzi ulionyesha kuwa katika nchi ya India rekodi yao ya Korosho
walizonunua kutoka Tanzania ilikuwa ni dola za kimarekani 120 milioni
kwa sababu wao walinunua tani 120,000 za korosho kutoka Tanzania. Hii
ina maana kuwa tani 40,000 hazikurekodiwa kwenye forodha zetu na hivyo
wauzaji kukwepa kodi ya ushuru wa korosho wa zaidi ya dola za kimarekani
12 milioni.
Pia kwenye kodi ya Mapato ya kampuni iliyouza korosho hizi mapato ya
zaidi ya dola 40 milioni hayatoonekana na hivyo kufanikiwa kukwepa kodi.
Huu ni mfano ninaopenda kuuleza katika kueleza namna mfumo wetu wa kodi
ulivyojaa matundu na kuhitaji kufanyiwa kazi kubwa ya kuufumua.
Kwa hiyo makampuni yana njia nyingi za kukwepa kulipa kodi na hivyo
wamiliki wake kujilimbikizia mali nyingi na kuongeza tofauti ya kipato
miongoni mwa wananchi. Kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tofauti ya
kipato itazidi kuongezeka na kuleta hatari kubwa kwa ustawi wa wananchi
na usalama wa nchi yetu.
Moja ya suala ambalo chama cha ACT Wazalendo ililieleza na halikuelezwa
na chama kingine chochote katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
ilikuwa ni hili la kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ili kila
anayepaswa kulipa kodi alipe kwa haki na kwa uwazi.
Tuliahidi "kuweka mfumo mpya wa kodi za kimataifa ili kuzuia makampuni
ya kimataifa kumomonyoa wigo wa kodi kwa kushiriki kikamilifu katika
kampeni za kimataifa za kurekebisha mfumo wa kodi za kimataifa, kupitia
mikataba ya kikodi na nchi nyengine ili kuzuia ukwepaji kodi na kujengea
uwezo kitengo cha kodi za kimataifa ili kudhibiti ukwepaji kodi".
Serikali ya Awamu ya Tano imefanya nini katika eneo hili?
Serikali ya Awamu ya Tano ilisifika kwa makusanyo makubwa ya kodi katika
miezi yake ya mwanzo ya kuongoza nchi yetu. Lakini haijafanya juhudi
yeyote ya ndani au ya nje kuhakikisha kuwa nchi inaondoa tofauti kubwa
ya kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho. Juhudi hizi za kukusanya
kodi hazijaweza kupunguza mzigo Wa kodi kwa wafanyakazi wa Tanzania.
Juhudi za kuendesha kampeni ya kimataifa ili kuboresha mfumo wa kodi za
kimataifa zimeshuka chini na kiukweli kama nchi tumerudi nyuma wakati
dunia nzima inashiriki kwenye kampeni hizi. Juhudi za ndani za kuongeza
makusanyo ya kodi kama hazitatazama mfumo wa kodi za kimataifa, basi
hazitakuwa na faida yeyote na tutabakia na kodi za wafanyakazi na
vibarua tu tukiwakamua zaidi ili kupata fedha za kuendesha nchi yetu.
Tunapendekeza nini?
1. Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi
zinazohusisha makampuni ya kimataifa (MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo
wa kodi ( Base Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni
hizi. Hili linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba
ya kikodi (double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi
nyingine duniani.
Tafiti mbalimbali katika eneo hili zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza 5%
ya Pato la Taifa kutokana na vitendo vya kampuni kubwa kukwepa kodi kwa
kutumia mbinu za kihasibu (tax planning measures). Serikali yetu
inapaswa kushirikiana na Serikali nyengine za nchi mbalimbali duniani
katika kampeni ya kimataifa ya haki za kodi (International Tax Justice
Movement).
Vyama vya Wafanyakazi nchini vinapaswa kuwa mbele kuishinikiza Serikali
kushiriki kwenye kampeni hizi na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye
sheria zetu za kodi ili kulinda wigo wetu wa kodi.
2. Serikali itazame upya michango ya wafanyakazi kwenye Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii. Viwango vya michango Kwa Tanzania vipo juu mno na
vinapunguza kipato cha mfanyakazi na kuongeza gharama kwa waajiri.
Michango ya Hifadhi ya Jamii ishushwe mpaka jumla ya 12% ya mshahara;
kwa Waajiri kuchangia 7% na Wafanyakazi kuchangia 5% ya mishahara yao.
Hii itasaidia kupunguza gharama za kuajiri kwa Waajiri. Vile vile Tozo
ya mafunzo SDL ishushwe mpaka 3% . Eneo hili ni muhimu liangaliwe kwa
muktadha wa kukuza ajira nchini hivyo ajira zinapoongezeka mapato kwenye
maeneo haya yanaongezeka pia.
3. Serikali idhibiti mfumuko wa bei kuhakikisha inapunguza gharama za
maisha kwa wafanyakazi. Katika wakati kama huu ambao bei za vyakula
zimepanda zaidi ya mara 2 kipato cha wafanyakazi wengi nchini kimebaki
palepale, hali hii inaongeza ugumu wa maisha kwao. Ni muhimu Serikali
kuchukua hatua mahsusi kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula nchini.
Mwisho, Wafanyakazi wa Tanzania, nawakumbusha kuwa kuna mahusiano chanya
kati ya maslahi yenu na aina ya uongozi wa kisiasa uliopo kwenye nchi.
Msikae pembeni kwenye harakati za mabadiliko ya kisiasa nchini. Vyama
vya Wafanyakazi vina nguvu zaidi ya kuhamasisha na kuweka mazingira
mazuri ya kidemokrasia na utawala wa kikatiba nchini.
Nawatakia Mei Mosi Njema.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Dar Es salaam.
Mei 1, 2017
Tags
Zitto Kabwe