RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Timu
ya Madaktari wabobezi kupitia Mashirika ya Peleks na Direct Aid Zanzibar kwa kuanzisha
utaratibu wa kuja Zanzibar kusaidia huduma za tiba.
Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo
Ikulu jijini Zanzibar wakati alipoagana na Timu ya Madaktari wabobezi kutoka
Mashirika Peleks na Direct Aids Zanzibar,
waliokuja nchini kwa ajili ya kusadia utoaji wa huduma za Afya.
Madaktari hao wabobezi kutoka nchi
za Saudi Arabia, Sudan, Misri na Romani wamefika nchini Mei 07, 2022 na kutoa
huduma hadi leo Mei 14, mwaka huu katika Hospitali
za Chake chake na Wete Pemba, ambapo jumla ya Operesheni za magonjwa mbali
mbali 190 zilifanyika.
Akizungumza na madaktari hao Dk.
Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamin juhudi na mchango
mkubwa wa wataalamu hao kwa kuzingatia kazi kubwa na nzuri waliyofanya kusaidia uimarishaji wa afya za wananchi kisiwani
Pemba.
Alisema hatua hiyo imesaidia
Serikali kupunguza gharama za kusafirisha
wagonjwa nje kwa ajili ya rufaa.
Alifahamisha hatua iliochukuliwa na
madaktari hao ni muhimu katika kuwajengea uwezo Madaktari wazalendo,
wauguzi na wafanyakazi wa Afya, kwa vile
walipata fursa ya kufanya kazi pamoja na wataalamu wabobezi.
Aidha, Dk. Mwinyi amefurahishwa
kupata tathmin kutoka kwa wataalamu hao
juu ya zoezi hilo lilivyokwenda kwa mafanikio makubwa.
Alieleza kuwa Serikali inaendelea
kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Afya nchini na
kusema inalenga kujenga Hospitali katika kila Wilaya zote na Mkoa ili kutoa
huduma bora za Afya, na hivyo kuwahakikishia wataalamu hao kufanya kazi katika
mazingira bora zaidi siku zijazo.
Dk.Mwinyi alitoa shukran kwa juhudi
na ukarimu mkubwa waliouonyesha wataalamu
hao na kuwataka kuendeleza imani waliyonayo na kuja nchini miaka ijayo.
Aidha, aliyashukuru Mashirika ya
Pellex na Direct Aid Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali na kudhamini
kambi hizo za utaoji tiba.
Nao kwa nyakati tofauti katika maelezo yao Madaktari hao; walimweleza
Rais Dk. Mwinyi kufurahishwa kwao kwa
kupata fursa ya kuja nchini kwa ajili ya kutoa huduma kwa ndugu zao wa
Zanzibar.
Walisema walifanyakazi wakiwa na
imani ya kuwasaidia ndugu zao wa Zanzibar, huku wakibainisha furaha waliyonayo
kutokana na ushirikiano na ukarimu
ulionyeshwa na Wizara, Madaktari na wauguzi pamoja na wananchi
waliowapatia huduma.
Madaktari hao wanaorejea nyumbani
baada ya kumaliza jukumu hilo, waliahidi kuwa mabalozi na kutoa taarifa njema
ya wananchi wa Zanzibar ili kuvutia Madaktari wengi zaidi kuja nchini siku
zijazo ili kazi hiyo iwe endelevu.
Sabamba na hilo waliahidi kutafuta
njia bora ili kupanua wigo wa utoaji huduma nyenginezo, pamoja na kujenga
mikakati na Serikali katika suala zima la upatikanaji wa vifaa vya tiba.
Nae, Mratibu wa Timu hiyo ya
Madaktari katika Hospitali ya Wete, Dr. Hawala Saleh alisema jumla ya
Operesheni 89 zilifanyika kwa mafanikio makubwa katika kambi hiyo ya siku saba
katika Hospitali ya Wete, huku Operesheni 101 zikifanyika Hospitali ya
Chakechake .
Aliyataja miongoni mwa magonjwa
yaliohusika na Operesheni hizo, kuwa ni Goita, Uvimbe katika kizazi, tenzi
dume, koo, korodan isioshuka, mifupa, vijiwe katika figo, uvimbe kwa mama
mzazi, uvimbe fuko la uzazi, mishipa pamoja na Ngiri.
Dr. Hawala alitumia fursa hiyo
kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omar kwa juhudi kubwa aliyofanya kufanikisha kambi
hiyo ya siku saba.
Aidha Mbunge wa Jimbo la Gando
(CCM) Salim Mussa Omar aliishukuru
Serikali kupitia Wizara ya Afya , Mashirika ya Pellix na Direct Aid Zanzibar
pamoja na timu hiyo ya Madaktari wabobezi kwa kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.
Alisema katika Jimbo la Uchaguzi
analolitumikia la Gando (Wilaya Wete), jumla ya wagonjwa 21 walifanyiwa
Operesheni mbali mbali, ambapo kiasi cha shilingi shilingi Milioni 84 ziliokolewa.
Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.