Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Qin Gang hajaonekana hadharani tangu mwishoni mwezi uliopita na kuzua tetesi juu ya uhusiano wake na mtangazaji maarufu wa televisheni.

Qin (57), mwanadiplomasia aliyeaminika na msaidizi wa karibu wa Rais Xi Jinping, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Desemba mwaka jana, akitokea kwenye nafasi ya balozi wa China nchini Marekani. Qin pia aliwahi kuwa balozi nchini Uingereza.

Mbali na ubalozi, Qin pia amepitia nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama cha Kikomunisti cha China (CCP), alijenga jina kwa ujasiri wake katika masuala ya kidiplomasia, hasa mikutano yake na maofisa wa serikali katika nchi za magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizozopo, Qin hajaonekana hadharani tangu Juni 25, 2023 alipofanya mkutano na mawaziri wenzake wa Sri Lanka, Vietnam na Urusi kwa nyakati tofauti, kwenye jijini Beijing.

Qin ambaye hupendelea kutabasamu alionekana akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Andrey Rudenko, aliyekwenda China kwa ajili ya mazungumzo kuhusu kundi la Wagner lililotaka kuasi nchini Urusi.

Hali hii si ya kawaida kwa waziri wa mambo ya nje kutoonekana hadharani kwa kipindi kirefu namna hiyo.

Hata hivyo, kuna taarifa zisizo rasmi kwamba waziri huyo amejihusisha kwenye mapenzi na mtangazaji maarufu wa televisheni, Fu Xiaotian (40), ambaye pia ameelezwa hajaonekana tangu waziri huyo alipotoweka.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China haikuwa tayari kuyatolea maelezo madai ya waziri huyo kutoweka.

Qin hakuonekana hata kwenye mikutano kadhaa ya kimataifa ukiwamo wa jumuiya ya mataifa ya kusini-mashariki mwa bara la Asia uliofanyika wiki iliyopita Jakarta nchini Indonesia huku taarifa za wizara zikisema ana “tatizo la kiafya.”